NA EMMANUEL MOHAMED
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema tatizo la
mfumo wa kununua umeme kwa njia ya mtandao limeshatafutiwa ufumbuzi na kwamba
wateja wataendelea kupata huduma hiyo.
Imeelezwa kuwa licha ya kupatikana kwa ufumbuzi huo, bado
mfumo huo utakuwa na kasi ndogo ya kuwahudumia wateja, ukilinganisha na awali.
Ofisa Uhusiano wa TANESCO, Adrian Mvungi, alisema tatizo
hilo linatokana na kutokea kwa hitilafu ya mfumo huo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wateja o wanaonunua umeme
kwa wakala wa vituo vya umeme.
Mvungi alisema juhudi kubwa zilifanywa kumaliza tatizo
hilo na kwamba mfumo wa huduma ya kununua umeme kwa njia ya mitandao jana
ilianza kufanya kazi.
"Tatizo hili ni
la nchi nzima, limewasumbua sana wateja wetu ambao wanatumia huduma ya kununua
umeme kwa njia ya LUKU, ikiwemo njia za miamala ya benki, kampuni za simu na
kwa njia ya max malipo," alisema.
Alisema kuna wateja ambao walituma pesa lakini
hawajapata ‘’tokeni” za kuingiza kwenye
mita, pia wapo waliopata tokeni, lakini hazikubali kuingia, hivyo mfumo haupo
katika kasi yake ya awali.
Aidha alisema kutokea kwa tatizo hilo hakuhusiani na
mabadiliko ya gharama za umeme kama baadhi ya watu walivyoanza kuzusha kwenye
mitandao mbalimbali ya kijamii.
Mvungi alisema TANESCO, wanatarajia kubadili mfumo wa
matumizi ya umeme, utakaokuwa wa kisasa, tofauti na unaotumika hivi sasa.
"Mfumo huu umepitwa na wakati ukilinganisha na mifumo
ambayo inatumika katika nchi zingine, hivyo TANESCO inatarajia kutumia mfumo mpya
kuanzia Aprili mwaka huu, ili kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa uhakika na kuondoa
usumbufu wa mara kwa mara,"alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru