Tuesday, 10 March 2015

Dewji abanwa mbavu



NA MARIAM MZIWANDA
BARAZA la Maadili ya Viongozi wa Umma, limemuhoji Meya wa Tabora, Gullam Dewji, kutokana na tuhuma za kutumia madaraka yake vibaya kwa maslahi binafsi, ikiwemo matumizi ya fedha za manispaa sh. milioni 2.6, alizotumia katika safari nchini Marekani.
Awali, akisomewa hati ya mashtaka na Mwanasheria wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, Dewji anatuhumiwa katika mashitaka matatu, likiwemo kutumia madaraka yake vibaya kwa kujinufaisha binafsi.
Dewji anadaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya safari nchini Marekani huku akijua wazi kwamba safari hiyo ilikuwa imedhaminiwa na kugharamiwa na wadhamini waliomualika kutembelea nchini humo.
Pia anadaiwa kushitakiwa kutumia nafasi ya meya vibaya kwa kujilimbikizia mali huku akijiua kuwa ni kosa kisheria.
Mali anazodaiwa kujilimbikizia Dewji  ni pamoja na viwanja vitatu vilivyopo maeneo tofauti katika Halmashauri ya Tabora, kikiwemo kiwanja namba 100 kitalu G eneo la Ipuli, kiwanja namba 158, kitalu G eneo la Ipuli, kiwanja namba 637, kitalu D eneo la Ipuli.
Kiwanja kingine ni namba 99, kitalu F eneo la Ipuli na kiwanja namba 206, kitalu C eneo la Usule.
Mali nyingine ni pikipiki 422, duka moja na magari matatu, moja likiwa na namba T 327 ADS, Toyota Hilux, T842 AWR, Toyota RAV 4, T110 CMW, Toyota RAV4.
Getrude alidai mshtakiwa hakuwahi kulieleza baraza hilo kuwa anamiliki mali zote hizo kwa kipindi cha miaka minne, yaani kuanzia mwaka 2010 hadi 2013.
Getrude aliongeza kuwa mMeya huyo amekuwa akitoa tamko la uongo kwa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kutoorodhesha mali hizo huku akijua wazi kufanya hivyo ni kosa.
Katika utetezi wake, Dewji alikana mashitaka yote na kulieleza baraza kuwa, suala la fedha alizozitumia kusafiri, mhusika mkuu ni Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kuwa ndiye aliyemlipa na yeye hahusiki katika masurufu.
Alisema anachojua fedha hizo alipewa kihalali kwa kufuata taratibu zote katika manispaa na kuongeza kuwa, amekuwa akituhumiwa kwa makosa hayo kutokana na msukumo wa kisiasa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi, lakini anamini yeye ni msafi na ataendelea kugombea nafasi ya udiwani bila kujali misukosuko anayokutana nayo.
Alisema fedha hizo alizichukua ikiwa ni katika utekelezaji wa mradi baada ya kuingia ushirikiano na Chuo cha Columbia ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizomo mkoani Tabora.
Dewji alisema katika mradi huo, halmashauri ilitakiwa kuchangia asilimia 17 kati ya milioni 200 ambazo zilipangwa kutumika.
Akizungumzia umiliki wa mali, alisema alikuwa akizimiliki kabla ya udiwani kutokana na kuwa mfanyabiashara kwa siku nyingi na shutuma zilizopo zimelenga kumchafua kisiasa kutokana na shughuli za maendeleo ambazo amekuwa akizifanya.

“Katika halmashauri yangu nimekuwa nikisimamia maendeleo, ikiwemo kuziba mianya ya ufisadi, ambayo madiwani walikuwa wakiifanya na kutokana na hali hiyo na nyakati za uchaguzi zilizopo, ndio matokeo ya chuki hizi,” alisema.

Alisema sababu nyingine ni wanasiasa wenzake kutaka kujijenga kisiasa, ambapo wapo wanaoutaka umeya, udiwani na wengine kumhofia kuwa huenda akagombea ubunge, jambo ambalo bado hajaamua kwa vile anasubiri wakati ufike ili afanye maamuzi sahihi.
Mmoja wa mashahidi aliyefika kutoa ushahidi wake  upande wa mlalamikaji, ambaye ni Diwani wa Isewe, Kaombwe Mrisho, aliomba ahakikishiwe ulinzi wake kwa madai kwamba maisha yake yapo hatarini.

“Mheshimiwa Jaji, naomba kwanza nihakikishiwe usalama wangu maana tunajuana namna tunavyoishi katika manispaa yetu na meya,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi  alimueleza shahidi huyo kuwa baraza lake sio kazi yao kumlinda mtu yeyote.
Jaji Msumi alihitimisha kikao hicho, kwa kusema kuwa wamefikia tamati ya kuwahoji viongozi wa umma na kufunga kikao chake.
Alisema wanatarajia kufikisha mapendekezo ya malalamiko yote yaliyosikilizwa kwa mamlaka husika ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kama sheria inavyowaelekeza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru