Na Willy Sumia, Sumbawanga
WAKATI Watanzania wakipaza sauti kukemea mauaji na ukataji viungo vya
albino, mtoto mwingine Baraka Cosmas (6), amevamiwa na kukatwa kiganja cha
mkono.
Tukio hilo ambalo limezidisha hofu miongoni mwa albino nchini, limetokea
usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Kipeta wilaya ya Sumbawanga mkoani
Rukwa. Habari za kuaminika zinasema kuwa, kundi la watu wasiojulikana walivamia kwenye nyumba aliyokuwa amelala Baraka na mama yake, Prisca Shaban na kuanza kuwashambulia kisha kukata kiganja hicho na kutoweka nacho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, watu hao walivamia nyumba hiyo wakiwa na mapanga na visu.
Alisema mbali na kukata kiganja cha Baraka, watu hao walimjeruhi sehemu mbalimbali za mwili.
Kamanda Mwaruanda alisema, wakati tukio hilo likitokea, baba mzazi wa mtoto huyo, Cosmas Yoramu (32), ambaye pia ni mlemavu wa ngozi, alikuwa amelala kwa mke mdogo.
Alisema watu watatu wanashikiliwa kwa kuhusika na tukio hilo na uchunguzi zaidi bado unaendelea huku hali ya Baraka, ambaye amelazwa kwa matibabu ikiendelea kuimarika.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku tano tangu Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, kuwahukumu watu wanne, adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la mauaji ya Zawadi Magindu (32), ambaye ni Albino.
Masalu Kahindi (54), Ndahanya Lumola (42), Singu Siyantemi (49), na Nassoro Saidi ambaye ni Mume wa marehemu, walimuua Zawadi kwa kumkata miguu, mkono wa kushoto kisha kutokomea nayo na kusababisha kifo chake papo hapo.
Februari 15, mwaka huu, mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati, aliuawa kwa kukatwa sehemu mbalimbali za viungo vyake na kisha mwili wake kutelekezwa kwenye msitu wa hifadhi ya Biharamulo, mkoani Geita.
Pia, mama mzazi wa mtoto huyo, Ester Jonas, anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Bugando mkoani Mwanza, baada ya kukatwa panga usoni wakati akijaribu kumuokoa mwanae.
Aidha, Oktoba 13 mwaka jana, Mughu Lugata (40), ambaye ni albino aliuawa kwa kukatwa kwa panga na watu wasiojulikana huku wakitoweka na baadhi ya viungo vyake.
Tukio hilo lililotokea Kitongoji cha Chalala, Kijiji cha Gasuma, Kata ya Nkololo, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, ambapo Lugata alikatwa mguu wa kushoto, vidole viwili vya mkono wa kushoto kisha kumyofoa kucha ya kidole gumba na kutokea na viungo hivyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru