Wednesday 25 March 2015

Kinana: Tusitegemee misaada kutoka nje



NA THEODOS MGOMBA, MOSHI.
WATANZANIA wameshauriwa  kutotegemea misaada kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo yao.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Moshi Vijijini, katika Kata ya Arusha Chini.
Kinana alisema hakuna mataifa kutoka nje ambayo yako tayari  kusaidia maenendeleo ya watu bila ya wao  kujitahidi kuondokana na umasikini.
Alisema tabia hiyo ya kutegemea misaada kutoka nje inawafanya Watanzania kuwa tegemezi na  kusababisha maendeleo kusua sua katika maeneo mengi.
Katibu mkuu alisema ni vyema Watanzania wakaachana na suala la kuwa ombaomba, badala yake watumie  zaidi nguvu zao katika kujiletea maendeleo yao.

"Sisi ni watu huru, hivyo ni lazima kutumia nguvu zetu kujiletea maendeleo yetu na si kuwa ombaomba, huko ni kuendelea kuwa tegemezi,” alisema.


Katibu mkuu  alisema hivi sasa taifa limepiga hatua kubwa katika masuala la maendeleo, hasa maeneno ambayo watu wake wameonyesha juhudi katika kujitolea.
Aidha aliwataka wakazi wa eneo hilo ambalo diwani wake ni wa kutoka upinzani, kuhakikisha kuwa katika uchaguzi mkuu ujao wanairejesha kata hiyo kwa CCM.
Alisema vyama vya upinzani vimekuwa vikiwadanganya wananchi ili kupata madaraka, huku vikiwa havina uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo.
Kinana alitoa mfano wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wilbroad Slaa, ambaye alidai angemlazimisha mmiliki wa kiwanda cha Sukari cha Moshi (TPC), awaongeze mishahara watumishi wa kiwanda hicho, jambo ambalo halikufanyika mpaka sasa.

"Achaneni na watu ambao wanaingia madarakani kutokana na kusema uongo, kiwanda hiki ni cha mtu binafsi, sasa utawezaje kumlazimisha kuongeza mishahara wewe mwanasiasa, wakati yeye mwenyewe hana uwezo huo?" alihoji Kinana.

 Katibu huyo alimwagia sifa mmiliki wa kiwanda hicho cha sukari kwa kuwa karibu na wananchi wa eneo hilo na kutoa misaada mbalimbali ya kijamii.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru