Thursday, 12 March 2015

Mapya yaibuka ajali ya Majinjah



  • Idadi ya waliokufa yaongezeka
  • Mbatia ajipanga kuchukua hatua

NA WAANDISHI WETU
IDADI ya watu waliokufa katika ajali iliyohusisha basi la Majinjah Express, kugongana uso kwa uso na lori, imeongezeka na kufikia 50.
Ajali hiyo iliyotokea juzi, Mufindi mkoani Iringa, ilisababisha kontena lililobebwa na lori hilo, kuangukia basi na kisha kuwabana abiria waliokuwemo na kusababisha vifo vya watu 42 papo hapo.
Hata hivyo, kumeibuka sintofahamu kuhusiana na idadi kamili ya watu waliokuwemo kwenye magari hayo, kutokana na idadi ya waliokufa kuwa kubwa tofauti na orodha iliyotangazwa awali. 
Aidha, kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Robert Salim, majeruhi mmoja aliyekuwa akitibiwa kwenye hospitali ya mkoa huo, alifariki usiku wa kuamkia jana.
Dkt. Salim alisema kati ya maiti 27, zilizopokelewa hospitalini hapo, saba zimetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa mazishi.
Waliotambuliwa ni Mbezi Deogratius (29), Editha Ngunangwa (28), Mohamed Juma (32), Ndenya Sixbert (25), James Kinyamaguho (30) , Said Halfan (35) na Abuu Mangula (35).
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema zoezi la utambuzi wa waliokufa linaendelea katika hospitali hiyo.
Kamanda huyo aliwataja watu waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo kuwa ni Mustafa Ally, Dominic Shauri, Tito Kyando, Martin Haule, Ipyana Mbamba, Fadhil Kalenga, Mussa Mwasege, Nehemia Mbuji, Josam Abel, Tumpate Mwakapala, Nico Hamis na Ester William.
Wengine ni Peter Mwakanale, Kelvin Mwakaladi, Raphael Nerbot, Maga Sebastian, Catherine Mwijungu, Lucy Mtanga, Debora Vicent, Ester na mwanaume, ambaye jina lake halikuweza kuitambulika kutokana na hali yake kuwa mbaya.
“Mpaka sasa majina ya watu waliotambuliwa ni hayo nane kwa kuwa, majina hayo tunayapata baada ya ndugu kuwatambua, tunafanya hivyo kutokana na baadhi ya abiria kutumia tiketi za abiria na baadhi yao kutoandika majina ya kweli,”alisema Kamanda Mungi.
Akizungumzia hali za majeruhi 13, waliolazwa kwenye hospitali ya wilaya ya Mufindi, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Boaz Mnenegwa, alisema  hali zao zinaendelea vizuri.
Aliongeza kuwa, Mtoto Kelvin Mwakaladi (9), ambaye ni miongoni mwa majeruhi hao, amekabidhiwa kwa maofisa wa ustawi wa jamii baada ya ndugu zake kutojitokeza kumchukua.
Wakizungumza na gazeti hili, majeruhi wa ajali hiyo, Catherin Mwijungu na Raphael Nerbot, waliiomba serikali kukifanyia ukarabati kipande cha barabara hiyo, hususani eneo la Changalawe kutokana na kuwepo kwa mashimo.
Pia, wameishukuru serikali kwa kuwapatia matibabu mazuri na kuwawezesha hali zao za kiafya kutengemaa.

MBATIA ATOA KAULI
MBUNGE wa Kuteuliwa, James Mbatia, anakusudia kupeleka mapendekezo ya kupitiwa upya kwa Sheria ya Usalama Barabarani, ili kuwepo kwa adhabu kali dhidi ya madereva wazembe wanaogharimu maisha ya watu kwa kusababisha ajali.
Pia ameiomba serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria, wale watakaobainika kuhusika na uzembe ulioasababisha ajali iliyotokea juzi, Mufindi mkoani Iringa, kati ya basi la Majinjah na roli, iliyoua watu 42 na wengine kujeruhiwa.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Mbatia alisema ajali zinazotokea nchini zinatokana na madereva kutozingatia sheria za barabarani na uzembe wa maofisa wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kushindwa kukarabati barabara zinapoharibika.
Alisema eneo la Changarawe, ambapo ajali hiyo ilitokea, sehemu kubwa ya barabara ina mashimo na kuwapa wakati mgumu madereva wengi pindi wanapofika eneo hilo.
Mbatia alisema licha ya ubovu huo wa barabara kufahamika, TANROADS wameshindwa kukikarabati kipande hicho, ili magari yapite kwa usalama, lakini madereva nao wameshindwa kuendesha magari yao kwa tahadhari.
“Kuna uzembe unaopaswa kutokufumbiwa macho kwa kuwa TANROADS walipaswa kukikarabati kipande hicho kwa wakati. Sambamba na hilo, madereva nao bado wanaendesha magari pasipokufuata tahadhari,” alisema.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI, alisisitiza kuwa, ili kuzuia ajali za namna hiyo, ni vyema kwa maroli ya mizigo kutembea usiku badala ya mchana kutokana na nyakati hizo mabasi ya abiria hayaruhusiwi kufanya safari zake.
Aliiomba serikali kuendelea kuimarisha usafiri wa reli, ambao utasaidia kupunguza mizigo mingi kusafirishwa kwa maroli, hali inayosababisha uharibu wa barabara. 
Alitaka kuwepo kwa utaratibu wa kutoa elimu kwa madereva, wafahamu thamani ya abiria wao, ikiwemo kufanyiwa uchunguzi kwa kila mwaka ili kubaini uwezo wao pindi wanapokuwa barabarani.
Aliwaomba wananchi kujenga utamaduni wa kutoa taarifa kwa vyombo husika, pindi wanaposhuhudia dereva anakwenda kinyume na  sheria za barabarani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru