Friday, 6 March 2015

TANESCO kuboresha uhusiano na watejaNA MOHAMMED ISSA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limeanzisha utaratibu wa kukutana na wateja wake kwa lengo la kujenga uhusiano mzuri baina ya shirika na wateja hao.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Usambazaji Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Sophia Mjema, alisema utaratibu huo utaboresha uhusiano baina ya shirika na wateja pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.
Alisema wameanza kukutana na wateja wakubwa na badae watakutana na wateja wa kati na wadogo ili kuongeza ufanisi na utendaji.
Sophia alisema hivi sasa shirika linahakikisha umeme unazalishwa kwa wingi na unawafikia wateja kwa wakati na kwamba lengo la TANESCO ni kwenda kibiashara zaidi.
Akizungumza kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika hilo kwa kampuni ya Helios Towers inayosambaza umeme kwenye minara ya simu nchini, Sophia alisema shirika litaendelea kuboresha huduma zake ili ziende na wakati.
Sophia alisema wateja wakubwa kama kampuni za simu zimefungwa mita maalumu ambazo zinasomeka moja kwa moja kwenye ofisi za TANESCO na kwamba mfumo huo umesaidia kudhibiti wizi wa umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa Helios Towers, Alexander High, alisema kampuni hiyo inauza umeme kwenye minara ya kampuni za simu nchini.
Alisema umeme huo wananunua kutoka TANESCO na kuuza kwenye kampuni hizo ambapo asilimia 70 ya minara inatumia umeme na asilimia 30 inatumia jenereta.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru