NA KHADIJA MUSSA
MTOTO mwingine wa Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, Magige Nyerere, amejitokeza na kuonyesha nia ya kuwania
urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Magige ni mtoto wa pili wa Mwalimu
Nyerere kuonyesha nia ya kuwania uras baada ya hivi karibuni Makongoro Nyerere,
kutajwa kuwa ni miongoni mwa watu wanaowania nafasi hiyo.
Mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere
amebariki watoto hao kuwania nafasi hiyo na kusema ni raia halali wa Tanzania
na wanayo haki ya kufanya wapendavyo bila ya kuvunja sheria za nchi.
Mama Maria yaliyasema hayo jana nyumbani
kwake Msasani, Dar es Salaam, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari ili kuwaondoa hofu wananchi juu ya uzushi
kuwa amefariki dunia.
“Makongoro ni mtanzania, naye ameamua kujitosa, anayo haki ya kufanya apendavyo bila ya kuvunja sheria. Magige naye aliniambia anataka kugombea urais nikasema vema,” alisema.
Hata hivyo, alikiri kuwa suala la kuwania
urais si jambo dogo, hasa kwa nchi change kwa sababu kuna mambo mengi muhimu ya
kuzingatiwa.
Akizungumzia kuhusu kuzushiwa kifo, Mama
Maria alisema zilimfurahisha kwa kuwa zilionyesha kuwa shetani ameshindwa,
amepata kipigo kutokana na sala na funga anazozifanya.
Hata hivyo, alisema watoto na familia
yake walihamaki na kuanza kumpigia simu wakitaka kuhakikishiwa juu ya jambo
hilo, ambapo alisema ni moja ya maajabu ya karne ya 21 kwa maerehemu kuongea
tena kwenye simu.
“Hakuna kitu kama hicho ni uzushi tu, hasa kinapofikia kipindi cha uchaguzi. Ni mambo ya makundi na hii si mara ya kwanza, watu wanatakiwa kufanya sana maombi kwa taifa ili damu isimwagike,”alisema.
“Nadhani watu walipokuwa hawajaniona UWT, nafikiri hata baada ya kuona mambo yanakwenda hovyo na nipo kimya, wakaona wanishtue,” alisema.
Aliwataja baadhi ya watu waliompigia simu
kuwa ni mke wa mtoto wake aliyeko Butiama, ambaye alikuwa amehamaki na kutaka
kujua nini kinaendelea. Mwingine ni Musuguri, ambaye alisema aliongea naye huku
akiwa anatetemeka.
Alisema uzushi huo, ambao unatokana na
masuala ya uchaguzi, uliongeza hofu kwa taifa, hivyo ameona ni bora ajitokeze
kwa sababu Watanzania wana hofu na ulimwengu nao una hofu.
Mama Maria ameishauri serikali itenge
siku maalumu kwa ajili ya kuliombea taifa.
Katika hatua nyingine, Mama Maria ametaka
suala la miiko ya uongozi lizingatiwe kwani hakuna taifa ambalo viongozi wake
hawana muongozo wa kimaadili
Alisema kutozingatiwa kwa miiko hiyo
ndiko kunakosababisha nyufa kwenye baadhi ya maeneo ya kiutawala na kiutendaji.
Mama Maria pia amelaani mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa kuwa yanamega furaha ya taifa na kuhoji
linakoelekea.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru