Thursday, 5 March 2015

Mwitiko wa serikali kuhusu maafa ya mvua Kahama...

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU

       TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

HATUA  ZA HARAKA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI KATIKA KUKABILI MAAFA YALIYOSABABISHWA NA MAFURIKO WILAYANI KAHAMA, MKOA WA SHINYANGA

Kufuatia mvua kubwa zilizonyesha usiku wa tarehe 04 Machi, 2015 Wilayani Kahama mafuriko makubwa yalitokea na kuathiri wakazi wa kata ya Mwakata katika vijiji vya Mwakata, Numbi na Mwaguguma.
Dk. Florens Turuka
Kutokana na mafuriko yaliyotokea tathmini ya awali inaonesha kuwa watu 42 wamepoteza maisha, watu 82 wamejeruhiwa na watu wanaokadiriwa kufikia 574 wameathirika. Jumla ya nyumba 137 zimeathirika kwa viwango mbalimbali.
Hatua zilizochukuliwa
Serikali imechukua hatua za haraka kwa kushirikiana na wananchi kuwafikia na kuwanusuru waathirika wa mafuriko hayo waliokuwa wamezingirwa na mafuriko. Aidha vimeanzishwa vituo vya muda kuwahifadhi wananchi hao  kwenye Shule.
Serikali imepeleka misaada ya kibinadamu kama ifuatavyo;
                     i.        Chakula tani 20. Maharage tani 5, Mafuta ya kupikia lita 1,126 na  Sukari tani 1.3
                    ii.        Vifaa vya matumizi ya ndani ambayo vinajumuisha blanketi 650,  ndoo 82 za lita 20, ndoo 82 za lita 10 ; Vifaa vya kupikia seti 82 na madumu 82

Kwa kuwa bado Serikali inalo jukumu kubwa la kuwawezesha waathirika kurejea katika maisha      yao ya kawaida; inapenda kuwatangazia wale wote wanaoguswa na         maafa haya kuwa Serikali inaendelea kupokea misaada mbalimbali ambayo inahitajika kwa waathirika.
Mahitaji haya ni pamoja na sare za shule; daftari za wanafunzi; mavazi ya kike na kiume; na chakula. Aidha kwa kuzingatia kuwa waathirika hawa wamepoteza mali na fedha katika maafa haya; misaada ya vifaa vya ujenzi (sementi, mabati, mbao, n.k.) inahitajika sana.
Utaratibu wa kupokea misaada hiyo kwa walio Dar es Salaam wanaweza kuiwasilisha misaada hiyo Idara ya Kuratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu au kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga_ Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Serikali itaendelea kuwasaidia Waathirika dhidi ya Changamoto zinazoweza kujitokeza hususani za kiafya zinazosababishwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira. Elimu juu ya ujenzi wa nyumba bora na makazi maeneo salama itaendelea kutolewa.

IMETOLEWA NA
Dkt. Florens Turuka
          KATIBU MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru