Thursday 12 March 2015

Naibu Waziri alia kufanyiwa fitina


NA THEODOS MGOMBA, CHEMBA
RAFU katika majimbo ya uchaguzi zimeanza kuwaweka mawaziri na manaibu mawaziri roho juu, ambapo safari hii ni zamu ya Juma Nkamia.


Nkambia, ambaye ni Naibu Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo na Mbunge wa Chemba, amelia kufanyiwa mchezo mchafu mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, 
Abdulrahman Kinana.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mjiro Juu, Nkamia alisema kuna watu wanatumia picha ya Rais Jakaya Kikwete na kudai amewatuma kuwania ubunge.
Alisema mmoja wa watu hao amekuwa akitumia picha aliyopiga na JK kama chambo na kuwaeleza wananchi kuwa ametumwa kuwania nafasi hiyo.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu huyo mtu anatembea na picha ambayo alipiga na Rais Kikwete na kuwaonyesha wananchi eti ametumwa kuja kugombea hapa Chemba.
“Inashangaza kama rais, mimi ndiye Naibu Waziri aliyenichagua na ninakaa naye meza moja kuzungumza naye kunapotokea umuhimu wa kufanya hivyo…sasa mimi na yeye nani yuko karibu na JK,” alihoji Nkamia.
Kwa upande wake, Kinana akizungumza na hadhara hiyo alisema muda wa kuanza kampeni bado na ni makosa kwa watu kuanza kujipitisha ama kushawishi wananchi.
Alisema ni vyema wabunge na madiwani wakaachwa wafanye kazi ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwani, muda wa kuifanya kazi hiyo bado upo.
“Nyinyi kamati za siasa ni lazima kuhakikisha hakuna mwanachama, ambaye kwa sasa anatembea kuwashawishi wananchi kumchagua wakati bado… waacheni wabunge na madiwani wamalize muda wao,” alisema
Kuhusu picha ya JK, Kinana alisema kutembea na picha sio tija kwa kuwa rais amepiga picha na watu wengi na wengine hawafahamu.
Akizungumzia suala la migogoro ya mipaka kati ya Mkoa wa Dodoma na ule wa Manyara upende wa Kiteto, Kinana alisema ni lalzima suala hilo sasa lifike mwisho.
Alisema hakuna sababu ya watanzania kuendelea kuuana kutokana na kugombea mipaka wakati wote ni watanzania.
Aliwataka wakazi wa Mrojo kuacha kudanganywa na kuchangishwa fedha na baadhi ya watu eti kwenda kumaliza mgogoro wa mipaka kati ya Dodoma na Kiteto.
Kinana alisema serikali imeshaanza kuchukua hatua kuhusiana na suala hilo na kwa sasa lipo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu likiendelea kushugulikiwa.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema suala la kuunda tume kushughulikia migogoro ya ardhi nchini kwa sasa lazima lifike mwisho.
Alisema kumekuwa na tume nyingi, lakini bado migogoro ya ardhi imekuwa ni sugu huku watu wakuwawa kila kukicha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru