Monday 16 March 2015

Kortini kwa wizi, utakatishaji fedha



NA FURAHA OMARY

MFANYAKAZI wa Benki ya CRDB, Telesphory Gura (43), amefikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kumwibia mwajiri wake sh. milioni 241 na kutakatisha fedha haramu.

Gura, mkazi wa Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam, alifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi.

Wakili wa Serikali, Genes Tesha, alimsomea Gura mashitaka matano ya wizi wa sh. 241,163,668 na ya kutakatisha fedha zaidi ya sh. milioni 130, anayodaiwa kuiyatenda kati ya mwaka 2008 na 2014.

Tesha alidai kati ya Agosti Mosi, 2008 na Machi 30, 2013 jijini Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa CRDB, aliiba sh. 48,085,254.45, mali ya benki hiyo.

Katika shitaka la pili, Gura anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2010 na Mei 30, mwaka jana jijini Dar es Salaam, aliiba sh. 62,667,549.73. Pia anadaiwa kati ya Machi Mosi na Septemba 10, mwaka jana, aliibia benki hiyo sh. 130,470,864.26.
Katika shitaka la nne la kutakatisha fedha, Tesha alidai kwamba kati ya Machi Mosi na Septemba 30, mwaka jana, mshitakiwa alihamisha sh. 117,196,000 kwa njia ya mtambo wa kieletroniki unaotumiwa makao makuu ya benki hiyo, kwenda kwenye akaunti ya Nyegina Tanzania Limited iliyoko CRDB Tawi la Azikiwe, Dar es Salaam.

Ilidaiwa mshitakiwa alifanya hivyo huku akijua kwamba fedha hizo hazijapatikana kwa njia halali na alikuwa na lengo la kuficha uhalisi wa zilikotokea.

Gura pia anadaiwa katika kipindi hicho, alihamisha sh. 13,274,864.26 kutoka akaunti ya CRDB kama sehemu ya kutayarisha mishahara kwenda akaunti ya Nyegina, huku akijua ni mazalia ya kosa la wizi.

Tesha alidai mshitakiwa alifanya hivyo kwa lengo la kuficha ukweli wa mahali zilikotokea fedha hizo.

Mshitakiwa alikana shitaka, ambapo Tesha alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Hakimu Moshi aliahirisha shauri hilo hadi Machi 30, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande kutokana na kosa la kutakakisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru