Wednesday, 25 March 2015

JK achochea upimaji virusiNA SULEIMAN JONGO, DODOMA
SERIKALI imempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuongeza hamasa ya upimaji virusi vya ukimwi na kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, aliyasema hayo jana bungeni mjini hapa wakati akiwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2014.
Alisema uamuzi wa Rais Kikwete na mkewe, Mama Salma Kikwete, kujitokeza hadhari kupima afya zao mwaka 2007, kuliongeza hamasa na kuchochea upimaji kwa hiyari.
Jenista alisema hatua hiyo iliongeza idadi ya watu wanaojitokeza kupima kwa hiyari kwenye vituo na maeneo mbalimbali yanayotolewa huduma hiyo nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Jenista, kabla ya Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete, kujitokeza hadharani na kupima afya zao, idadi ya waliopima kwa hiyari ilikuwa ni watu milioni 2.2 pekee.
Alisema baada ya Rais Kikwete kutoa hamasa hiyo, idadi ya waliojitokeza kupima kwa hiari hadi Desemba, mwaka 2014, ilikuwa ni watu 25,468,564.

"Tunampongeza Rais kwani hivi sasa suala la kupima kwa hiyari kwa Watanzania ni la kawaida. Si ajabu wala hakuna woga kwa Watanzania kwenda kupima," alisema.

Akizungumzia madhumuni ya muswada huo, alisema unalenga kuongeza mapambano zaidi.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, alisema kumekuwepo changamoto katika utekelezaji wa shughuli za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), unaochangiwa na upungufu uliopo kwenye sheria iliyoanzisha tume hiyo.
Alisema wakati sheria hiyo ilipotungwa, iliandaliwa katika mazingira kama ni jambo la dharura, lakini hadi sasa ni miaka 30 imepita na tatizo liko palepale.
"Kutokana na upungufu mbalimbali, serikali imeona ni vyema kuleta marekebisho haya ili kuiongezea nguvu katika mapambano hayo," alisema.
Katika muswada huo, serikali imependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Ukimwi, utakaokuwa na  uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na tatizo hilo.
Akichangia muswada huo, Diana Chilolo (Viti Maalum- CCM), alisema licha ya TACAIDS kufanya kazi kubwa, serikali imekuwa ikichangia asilimia tatu tu ya fedha za mapambano dhidi ya ukimwi.
Alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kutasaidia kufungua mlango zaidi kuweza kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Naye Maria Hewa (Viti Maalum- CCM), alisema aliunga mkono pendekezo la kuzitaka halmashauri ziwe na mifuko inayoweza kushughulikia masuala ya ukimwi kuanzia kwenye halmashauri.
Aidha, alipendekeza sheria hiyo iwe na kipengele kitakachodhibiti matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya mapambano dhidi ya ukimwi.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya,  Kamishna Msaidizi Godfrey Nzowa, amesema mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya nchini, yanahitaji uadilifu na weledi miongoni mwa viongozi, wanausalama na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na Uhuru kuhusiana na sheria mpya iliyopitishwa na  Bunge, Nzowa alisema kitendo kilichofanywa na wabunge ni cha kupongezwa na ni wajibu wao kutunga sheria mpya, kuzifanyia marekebisho na kuziondoa sheria zinazoonekana hazina tija kwa wakati husika ili kuleta maendeleo endelevu ya taifa kiuchumi.
Alisema adhabu zilizowekwa za sh. bilioni moja au kifungo cha miaka 30 jela kwa watakaokamatwa huku wasafirishaji wakiandamwa na kifungo cha maisha, zinaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa biashara haramu ya dawa za kulevya endapo uadilifu utakuwepo.
Alisema uadilifu kwenye mapambano ya dawa za kulevya ndio msingi wa mafanikio, hata ziwepo sheria kali kiasi cha kutisha, kutokana na uwepo wa fedha nyingi kwenye mtandao wa biashara hiyo, jambo linalosababisha tamaa kwa baadhi ya watendaji wa vyombo vya usalama, viongozi na wananchi kwa ujumla.

“Kwa uzoefu wangu, uadilifu ndio kila kitu kwenye mapambano haya. Sheria kali sawa ziwepo, ila kila mtu kwa nafasi yake azingatie weledi kwenye kila hatua anayoichukua kuwafikisha wahalifu mikononi mwa sheria kwa sababu fedha zinawapa tamaa watu wengi,” alisema Kamishna Nzowa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru