NA THEODOS MGOMBA, VUNJO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema wananchi wanaochagua upinzani kuongoza katika maeneo yao hawaiadhibu CCM, bali wanajiadhibu wenyewe.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo juzi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Vunjo.
Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidhani kuwachagua wapinzani katika maeneo yao ni moja ya njia ya kuiadhibu CCM.
Alisema mawazo hayo ni potofu, kwani vyama wanavyovichagua havina serikali inayoiongoza, wala mawaziri.
“CCM ndiyo yenye serikali, yenye mawaziri na hata wakuu mbalimbali wa idara, ambao ndiyo wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo na si viginevyo.
“Inashangaza kuona mtu anachagua upinzani kwa kudhani eti anaiadhibu CCM, hii si kweli, kwani hata hao wapinzani ndani ya Bunge ni wachache kuliko wa CCM,” alisema Kinana.
Alisema hivi sasa wapinzani wameunda umoja unajulikana kwa jina la UKAWA ili kukusanya nguvu.
Kinana alisema pamoja na kuunda umoja huo, bado wapinzani kila mmoja anataka kuongoza au kutoa mgombea wa nafasi mbalimbali, ikiwemo ya urais.
“Sasa kila mmoja anataka kugombea urais wakati walishakubaliana kuwa watakuwa na mgombea mmoja, hii inaonyesha kuwa watu hawa wana uroho wa madaraka na si kuwatumikia wananchi,” alisema.
“Nataka kuwaambia ndugu zangu kuwa katika uchaguzi mkuu ujao, CCM itashinda kwa kishindo na huo UKAWA utageuka na kuwa UKIWA, hivyo mnaopigia upinzani mjiandae kuwa wakiwa,” alisema.
Katibu Mkuu aliwaasa wakazi wa jimbo hilo kuacha kuchagua viongozi wao kwa majaribio, kwani kwa kufanya hivyo wanajikosesha maendeleo.
Thursday, 26 March 2015
Wasioichagua CCM wanajikomoa
03:55
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru