Wednesday, 11 March 2015

Nyalandu azindua ofisi za TAWA


Na mwandishi wetu MAMLAKA ya Wanyamapori Tanzania (TWA), imepata ofisi za muda mkoani Morogoro, kwa ajili ya matumizi ya muda, hivyo kuanza kazi wakati wowote kuanzia sasa. Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alitembelea ofisi hizo zitakazokuwa kwenye jengo la Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) jana, alipokuwa na kikao cha kupitisha bajeti ya mamlaka hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu. Alikipongeza kikosi kazi kinachosimamia uanzishwaji wa TAWA kwa kufanya kazi kwa bidii na kuahidi kazi rasmi zitaanza baada ya kuteuliwa kwa mwenyekiti wa bodi.
Tayari wajumbe wa bodi ya mamlaka hiyo wameshapatikana na kinachosubiriwa ni Rais Jakaya Kikwete kumteua mwenyekiti.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori, Anthony Klerio, alieleza kuwa kasi ya ujangili nchini imepungua ingawa kuna changamoto katika baadhi ya maeneo. “Kuna maeneo ambayo kwa sasa ujangili umekuwa ukifanyika kwa uharibifu mkubwa kwani, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia bodaboda katika kuwinda Twiga na Pundamilia kwa kuwakata miguu kwa panga,”alisema. Alisema ujangili wa namna hiyo unakuwa vigumu kutambulika kwani hufanyika kimyakimya, tofauti na watu wanaotumia risasi kwani, kunakuwa hakuna milio na hivyo kufaya maaskari kushindwa kutambua iwapo kuna majangiri porini. Alisema hali imekuwa mbaya kwa mapori yaliyo karibu n mipaka ya nchi jirani, hususan kwa maeneo ya pori la Rukwika wilayani Masasi, na kuongeza kuwa, kwa upande huo hali ya tembo sio shwari na kwamba, maeneo mengne hatari ni mikoa ya Rukwa, Katavi na Tabora. Nyalandu alisema serikali imejitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha vita dhidi ya ujangili inakuwa endelevu na kwamba, mamlaka hiyo pindi itakapoanza kazi, itajengewa uwezo zaidi.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru