Tuesday, 10 March 2015

EWURA yaagizwa kupunguza zaidi bei ya mafuta


NA WAANDISHI WETU

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetakiwa kuhakikisha inaendelea kupunguza bei ya mafuta kulingana na mabadiliko katika soko la dunia.
Agizo hilo limetolewa jana na Kamati ya PAC wakati ilipokutana na watendaji na maofisa wa EWURA, ambapo imesema ni lazima bei ya mafuta nchini ibadilike kulingana na bei ya soko duniani.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Ismail Aden Rage, alisema bei ya mafuta kwenye soko la dunia imepungua kwa asilimia 25, hivyo mamlaka hiyo iendelee kupunguza bei ili kila Mtanzania afaidike.

“Ewura ni lazima wapunguze bei ya mafuta kulingana na mabadiliko ya soko, tunajua hivi sasa bei ipo chini, lakini inatakiwa ipungue zaidi kulingana na soko hilo,” alisema Rage.

Aliitaka EWURA kujenga jengo lao ili kupunguza  gharama wanazotoa katika jengo walilopo sasa.
Alisema hivi sasa mamlaka hiyo inalipa shilingi bilioni 1.2, kwa ajili ya kulipia pango kila mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa.
Alisema hivi sasa mashirika ya umma yamejenga majengo mengi ya kisasa, hivyo ni bora kuhamia katika majengo hayo kwa kuwa bei ya pango si kubwa kama ilivyo katika majengo ya watu binafsi.
Vilevile aliitaka Mamlaka hiyo iwe makini katika utoaji wa vibali wa ujenzi wa vituo vya mafuta karibu na makazi ya watu.
Akijibu mapendekezo yalitotolewa na Rage, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Simon Sayore, alisema watashusha bei ya mafuta kulingana na muelekeo wa mabadiliko kwenye soko la dunia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru