Saturday, 14 March 2015

Kinana Katibu Mkuu wa aina yake-Lowassa


MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa, amesema uongozi wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ni wa aina yake na ambao haujapata kutokea.
Alisema kasi hiyo haijawahi kutokea kwa makatibu wakuu waliopita na hivyo kummwagia sifa Kinana kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukitumia Chama.
Lowassa alisema hayo juzi alipokuwa akitoa salamu za jimbo hilo mara baada ya kuwasili kwa Kinana na ujumbe wake katika Kijiji cha Oloksale.
Alisema endapo wabunge wote wa CCM wangetekeleza Ilani ya Chama hakungekuwa na sababu ya Kinana kutembea nchi nzima kuimarisha Chama.
Mbunge huyo alisema yeye binafsi anashangazwa na kasi anayofanya na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye katika kukiimarisha Chama nchi nzima.
Lowassa alisema hivi sasa Kinana anatembea nchi nzima kuimarisha Chama, kazi ambayo kama kila mbunge angetimiza wajibu wake asingeifanya.
ìMimi nadhani wewe ni katibu mkuu wa kwanza kufanya kazi nzito ya kuzunguka nchi nzima kukiinua Chama, nakupongeza sana wewe na Nape kwa kazi nzuri mnayofanya,îalisema.
Lowassa alisema katika jimbo lake amejitahidi kutimiza Ilani ya CCM kwa kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo hata kwa kutumia fedha zake.
ìSisi hapa tumejenga shule, tuna maji ya kutosha na hata hospitali ya wilaya na kama wabunge wengine wangefanya hivyo,îalisema.
Aidha, alikiomba Chama kuangalia utaratibu wa kuunda tume maalumu ya Chama kuchunguza migogoro ya wafugaji na wakulima.
Alisema Chama kiliwahi kuunda tume kama hiyo miaka ya 1980 kuchunguza mauaji ya wazee kwa imani ya kishirikina na iliweza kufanya kazi nzuri na kukomesha mauaji hayo.
ìIle tume ilikuwa ikiongozwa na mama Mongela (Getruda) wakati ule iliweza kuleta suluhisho la wazee wakawa salama,îalisema.
Mbunge huyo alisema ni vyema sasa CCM ikatafakari juu ya kuunda tume kama hiyo ili iweze kuleta suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Kinana alimpongeza Lowassa kwa kuwatumikia wananchi wake na kutekeleza kikamilifu Ilani ya uchaguzi ya CCM.
Pia alimpongeza Lowassa kwa uamuzi wake wa kustaafu kwa hiari nafasi ya ubunge.
Alisema ingawa amesema hatagombea tena, lakini wakazi wa Monduli watamkumbuka kwa mambo mengi aliyowafanyia.

1 comments:

  1. Kinana na Nape ni majembe hasa ndani ya Chama Chetu na Lowassa ni jembe la maana katika nchi yetu.

    ReplyDelete