Tuesday, 10 March 2015

Tanroads yafafanua matumizi ya bil. 252/-                                                                                    NA EMMANUEL MOHAMED
Mhandisi Mfugale Patrick
MKURUGENZI wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi, Patrick Mfugale, amesema fedha zilizodaiwa kuibwa TANROADS, zilitumika kulipia madeni ya wakandarasi kinyume na ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Mfugale amesema pesa hizo zilitolewa kwa ajili ya miradi mipya, lakini zikatumika kulipa madeni yaliyokuwa yanadaiwa na wakandarasi.
Kigogo huyo wa TANROADS alitoa ufafanuzi huo jana baada ya kuwepo na taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, zikidai kuwa umefanyika ufisadi wa sh. bilioni 252.

 “Sijawahi kuitisha mkutano na waandishi wa habari, lakini leo (jana) nimefanya hivi kutokana na kuona kwenye baadhi ya magazeti kuwa kuna ufisadi mkubwa wa pesa hizi. Nasema kuwa hakuna ufisadi wowote unaohusishwa na fedha hizi,”alisema.

Mfugale alisema fedha hizo zilishatolewa ufafanuzi na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, lakini anashangaa kuona suala hilo limeibuliwa upya.

 “CAG akiwahi kuhoji kuhusu fedha hizo, ambazo zimeonyeshwa kwenye taarifa ya hesabu za Wizara ya Ujenzi kama vile miradi mipya ya mwaka 2011/2012, tofauti na uhalisia wenyewe ulivyokuwa,” alisema.

Alisema baada ya fedha hizo kupokewa na Wizara ya Ujenzi kutoka hazina, zilihamishwa kwenda TANROADS kwa ajili ya kulipia madeni ya wakandarasi wa miradi ya barabara, ambao hawajalipwa mwaka wa fedha 2010/2011.
Alisema fedha hizo zilijumulishwa kwenye hesabu za wizara kama matumizi ya akaunti ya maendeleo na hivyo kuongeza matumizi ya wizara kimakosa. Alisema zilitakiwa kuonyeshwa kwenye hesabu za mtumiaji halisi, ambaye ni TANROADS .
Alisema kutokana na kosa hilo, wizara ilipewa hati ya ukaguzi yenye mashaka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru