Tuesday 10 March 2015

Kigogo CCM akana kupewa onyo

NA ANITA BOMA, IRINGA
KUMEIBUKA sintofahamu kuhusiana na hatima ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, anayedaiwa kuadhibiwa na Kamati ya Maadili kutokana na madai ya kukihujumu chama chake.

Awali, ilielezwa kuwa Jesca amepewa adhabu ya kusimamishwa uanachama, lakini baadaye ikabainika kuwa amepewa onyo kali kuhusiana na tuhuma hizo.

Hata hivyo, Jesca ameibuka na kueleza kuwa amekata rufani kupinga hatua zilizochukuliwa dhidi yake na kusisitiza kuwa uamuzi huo haukuzingatia sheria na kanuni za Chama.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juzi, Jesca ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kitanzini/Miyomboni, alisema amepinga uamuzi huo uliochukuliwa dhidi yake.

Alisema uamuzi huo haukuzingatia kanuni za uongozi na maadili ya CCM Ibara ya 93 (15) na Ibara ya 95 (7).

Kwa mujibu wa Jesca, ibara hizo zinaelezea taratibu za kusimamishwa uongozi, kiongozi yeyote wa ngazi ya wilaya iwapo atadhihirika kuwa na tabia na mwenendo utakaomwondolea  sifa za uongozi.

“Ingawa wilaya ya Iringa Mjini kupitia Katibu wake, Zongo Lobe Zongo wamenipa adhabu, mimi ni mwenyekiti wa mkoa, natakiwa kupewa onyo kali na kuelezwa taratibu zingine zitafuatwa kwa mujibu wa vikao.

“Kitendo hicho kimeleta uvumi mkubwa wa kuwa nimesimamishwa uanachama na kuvuliwa nafasi zote za uongozi kwa madai nimekisaliti Chama. Hii  si kweli, na hata mamlaka iliyoamua hilo hawakufuata taratibu na kanuni za maadili ya uongozi kwani, kwa nafasi yangu siwezi kusimamishwa uongozi na ngazi ya mkoa…hata pia kwa nafasi yangu ya diwani, lazima ipelekwe vikao vya ngazi ya taifa,” alisema Jesca.

Alizitaja baadhi ya sababu zilizodaiwa kusababisha kupewa onyo kali, kuwa ni kumsaidia mgombea wa CHADEMA kushinda katika uchaguzi wa serikali za mtaa, kuzuia watu wasivae sare za CCM na kuhamasisha wapinzani kujiunga kwenye VICOBA vya CCM.

Hata hivyo, Jesca alisema mtaa ambao anatuhumiwa kumsaidia mgombea wa CHADEMA haufahamu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alisema madai ya Jesca hayana ukweli na kamwe halmashauri kuu ya mkoa haiwezi kumuondoa madarakani.

Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ndiyo yenye jukumu la kumvua wadhifa huo.

Alisema Kamati ya Maadili ya Iringa Mjini ndio iliyompa adhabu Jesca kutokana na tuhuma walizoziona dhidi yake na si mkoa kama inavyodaiwa.

“Ni kweli ilitangazwa katika kikao cha siasa na maadili ndiyo imempa onyo kutokana na wao kubaini anafanya vitendo kinyume maadili ya uongozi wa CCM, hakuvuliwa madaraka kwa kuwa wilaya haina uwezo wa kufanya hivyo,” alisema Mtenga.

Naye Zongo alisema uongozi wa wilaya una mamlaka ya kumwadhibu mwanachama na kiongozi wa ngazi ya kata kwa kukiuka taratibu za kimaadili kulingana na kosa alilotenda na si kumvua wala kumuachisha kiongozi wa mkoa nyadhifa zake kwani, hayo ni maamuzi ya ngazi za juu na si wilaya.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru