Tuesday, 10 March 2015

Sitta atoa siku 6 kwa vigogo TRLNA MOHAMMED ISSA
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameipa siku sita Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRL), kuwasilisha taarifa ya mabehewa ya mizigo yanayodaiwa kuanguka ili hatua ziweze kuchukuliwa mara moja.
Samuel Sitta
Pia ameitaka Bodi ya TRL, kueleza taratibu zilizotumika kununuliwa mabehewa hayo ambayo yanadaiwa si mapya.
Alisema ni lazima watakaobainika kufanya uzembe katika mchakato wa manunuzi ya mabehewa hayo wawajibike.
Mbali na hilo, Sitta aliagiza mabehewa 124, ambayo yako India yasiletwe nchini mpaka yatakapobainika ubora wake.
Alisema mabehewa yaliyonunuliwa na TRL ni 274, ambapo 150 yameshafika nchini na yaliyobaki ameamuru yabaki India.
Sitta alitoa agizo hilo jana mjini Dar es Salaam, mara baada ya kukutana na bodi ya shirika hilo.
Alisema ameiagiza bodi hiyo kuwasilisha taarifa ya mabehewa hayo Jumatatu ijayo ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Sitta alisema mabehewa hayo yanadaiwa kuwa si mapya na kwamba ndio sababu yakawaka yanaanguka mara kwa mara.
Alisema Desemba, mwaka jana, upindukaji wa mabehewa uliongezeka na kusababisha athari kwa reli.
Sitta alisema wakati umefika watumishi wanaofanya uzembe kuwajibika ili kukomesha uzembe sehemu za kazi.
Hata hivyo, aliipongeza menejimenti ya TRL kwa kuongeza mapato na kulifanya shirika kuimarika.
Alisema wizara hiyo itahakikisha mishahara ya watumishi inapatikana kwa wakati kama walivyoahidiwa.
Sitta alisema mapato ya shirika hilo yatazidi kuongezeka kutokana na kupata vifaa vipya na vya kisasa.
Alisema idadi ya treni za kwenda Bara itaongezeka na kwamba, lengo ni kuimarisha huduma ya usafiri wa treni.
Sakata lilivyokuwa
Desemba mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa sita wanaodaiwa kuisababishia hasara kampuni hiyo kwa kushindwa kuhakiki ubora wa mabehewa ya mizigo yaliyonunuliwa na serikali.
Aliwataja maofisa hao, ambao ni wahandisi kuwa ni Pascal, Ngoso, Kaukunda, Chambika, Lugela na Kessy, ambapo barua zao za kusimamishwa kazi walikabidhiwa Desemba 10, mwaka jana.
Aliongeza kuwa pamoja na uamuzi huo kufikiwa, bodi ya zabuni ya TRL imevunjwa na tayari mchakato wa kuundwa kwa bodi mpya umeanza.
Kufuatia sakata la ubovu wa mabehewa ya mizigo na kusababisha kuanguka pindi yanapokuwa safarini, Dk. Mwakyembe aliunda kamati ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Bodi ya Wahandisi, TRL huku akimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kuongeza wataalamu wawili kufuatilia ubora wa mabehewa hayo.
Alisema kamati hiyo itakwenda nchini India kwenye Kampuni ya Hindu Stant, kuhakiki ubora wa mabehewa hayo na pindi ikibainika kuwa hayakutengenezwa kulingana na viwango vinavyokubalika, serikali itachukua hatua za kisheria.
Gharama za mabehewa
Serikali ililipa zaidi ya sh. bilioni 45, ikiwa ni gharama za ununuzi wa mabehewa 274, ambayo ni wastani wa milioni 166 kwa kila behewa.
Lengo la serikali lilikuwa kuiwezesha TRL, kusafirisha mizigo tani milioni 1.5 kwa mwaka na kuiwezesha kampuni hiyo kujiendesha kwa faida.
Mabehewa hayo yalikuwa ya aina tatu, ambayo ni ya kubebea makasha, mizigo kichele na mafuta.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru