Thursday, 12 March 2015

CCM yalalamikia ucheleweshaji wa fedha za miradi


NA THEODOS MGOMBA, KONDOA
SERIKALI imeshauriwa kutoa fedha kwa wakati kwenda katika halmashauri baada ya bajeti yake kumalizika.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Gwandi kilichoko wilayani Chemba mkoani Dodoma.
Kinana alisema kumekuwepo na ucheleweshaji wa miradi mbalimbali ya serikali kutokana na fedha kutofika kwa wakati katika halmashauri nyingi.
Alisema hali hiyo imekuwa ikirudisha nyuma kasi ya maendeleo katika maeneo husika kwani hata fedha zinapofika, huwa ni kidogo na hazilingani na mgawo halisi.
“Kuna tatizo la kuja kwa fedha kutoka serikali kuu na mara nyingine huja kidogo au zisifike kabisa, hili nalo ni tatizo,” alisema Kinana.
Aliongeza kuwa CCM ndicho Chama pekee, ambacho kimepewa dhamana ya kuisimamia serikali, hivyo kitahakikisha serikali inatoa fedha kwa wakati.
Aliwataka wananchi wa Gwandi kuendelea kukiamiani na kukichagua Chama cha Mapinduzi kwani ndicho pekee kinachotekeleza Ilani yake hapa nchini.
Alisema hakuna Chama kingine chenye wajibu wa kufutilia maendelea na hali ya wananchi wake kwani vyote havina ilani inayotokelezwa na serikali.
“Naomba muendelee kuiamini CCM kuwa ni chama pekee kinachoweza kuwasaidia katika shida zenu na si vyama vingine kwani hivyo havina Ilani, achaneni navyo,” alisisitiza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru