NA EMMANUEL MOHAMED
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuharakisha malipo ya fidia kwa
wananchi wa eneo la Kipunguni, Dar es Saalam kabla ya kuanza kwa vikao vya Bajeti
vya Bunge.
Imesema kuendelea kucheweleshwa kwa juhudi za kulipa
fidia hiyo inahatarisha kusitishwa kwa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria
(Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Awali, wananchi wa eneo hilo walitakiwa kulipwa kiasi
cha sh. bilioni 11, lakini kutokana kuchewelewa huko na mabadiliko ya taratibu
ya sheria ya mpya ya fidia ya ardhi mwaka 1997 imeongezeka na kufikia sh. bilioni
18.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Juma Kapuya alisema
deni hilo ni kubwa na kwamba kuchewelewa kulipwa pesa hiyo kutachangia kuanza
kuteteleka kwa utekelezaji wa mradi huo.
Kapuya alisema kamati hiyo itajitahidi kufanya
mawasiliano ya karibu na Serikali ili kutafuta pesa hizo na kuanza kuwalipa kwa
wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi
Suleman Suleiman, alisema deni hilo ni miongoni mwa changamoto zinazoikumba
utekelezaji wa mradi huo.
Mbali na hilo, pia utafiti unaonesha kuwa ifikapo
2020, miaka mitano kuanzia sasa abiria watakao kuwa wanatumia kiwanja hicho
watakuwa zaidi ya milioni tano hivyo changamoto kubwa ni kuunganishwa kwa
utekelezaji wa awamu ya kwanza na ya pili kwa pamoja.
“Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha deni hilo linalipwa kwa wakati asilimia 15 ya gharama za mradi inalipwa na TAA kupitia tozo la abiria ambayo hupitia hazina na kurejeshwa huku lakini bado pesa hizi zinachelewa na kuletwa kidogo kuliko makusanyo mpaka sasa tumeshawalipa bilioni moja tu,” alisema.
Naye Zerina Madabida, aliwataka TAA kutafuta vyanzo
mbalimbali vya mapato ikiwemo TRA,Hazina na mashirika mengine ya Serikali ili
kuharakisha fidia hiyo na kuondokana na usumbufu huo.
Zalina alisema
kuendelea kwa tabia za kuchelewesha fidia inachangia kuharibika kwa
miradi kama hiyo yenyec faida kubwa kwa taifa ikiwemo barabara, viwanja vya
ndege na majengo.
Aidha, kamati hiyo imeisifia hatua inayoendelea kwa
ujenzi huo ambao unagharimu sh. bilioni 518, huku awamu ya kwanza unagaharimu
bilioni 293 na awamu ya pili itagharimu sh. bilioni 225.
Pesa hizo ni mkopo kutoka benki ya HSBC ya uingereza
kwa asilimia 85 kwa dhamana ya serikali ya Uholazni kupitia Export Credit
Agency na Benki ya CRDB kwa asilimia 15.
Asilimia 30 ya ujenzi huo itajikita katika majengo ya
kibiashara ikiwemo maduka na hoteli ili kuasaidia kukua kwa uchumi wa taifa na
kukua kwa uchumi kwenye sekta ya anga pia itawanufaisha watanzania katika fursa
ya ajira.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru