Tuesday, 17 March 2015

VITA YA UJANGILI


Serikali yapewa  ndege ya kisasa

NA KHADIJA MUSSA
WADAU wa utalii na uhifadhi ndani na nje ya nchi wameendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya ujangili, kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.


Tangu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kutangaza vita dhidi ya ujangili na kusisitiza kuwa lazima serikali ishinde, matukio ya mauaji ya tembo na faru yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Hiyo inatokana na kuimarishwa kwa ulinzi kwenye hifadhi za taifa pamoja na serikali kusambaza vifaa vya kisasa kwa askari wa wanyamapori ili kuhakikisha inasambaratisha mtandao wa ujangili nchini.
Ni katika kuunga mkono jitihada hizo, Nyalandu amepokea msaada wa ndege ndogo aina ya Micro light Nyinja 5H-HEL yenye teknolojia ya hali ya juu katika kukabiliana na ujangili.
Ndege hiyo iliyotengenezwa kisasa, imetajwa kuwa na uwezo wa ziada tofauti za zingine ikiwemo kuona na kukusanya taarifa za matukio yote yanayoendelea kwenye maeneo inayopita.
Ndege hiyo mpya yenye thamani ya dola 220,000 (sh. milioni 410) imetolewa na Mwenyekiti wa Tanganyika Wildlife Safaris, Eric Pasanisi, kwa ajili ya kupambana na ujangili katika Pori la Akiba la Selous.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Nyalandu, alisema msaada huo unalenga kuimarisha vita dhdi ya ujangili nchini.
Alisema ndege hiyo yenye uwezo wa kutembea mwendo mdogo ikiwa angani, itasaidia kuona majangili na kuwashughulikia, hivyo kuimarisha usalama wa wanyamapori na rasilimali za misitu nchini.
“Ndege hii mpya mbali na kutembea mwendo mdogo pia imetengenezwa kwa usalama wa hali ya juu kwa sababu ina ‘parachute’ ambayo inaweza kuishusha hadi chini iwapo itapata hitilafu kwenye injini ikiwa angani,” alisema.
Kwa upande wake, Pasanisi alisema ndege hiyo itakuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na ujangili nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru