Thursday, 26 March 2015

CCM yaitaka serikali kuacha urasimu


SERIKALI imeshauriwa kupunguza urasimu wa ufanyaji biashara katika maeneo ya mipakani, ili wananchi wengi  watumie fursa hiyo katika kujiongezea kipato.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Himo.
Alisema Tanzania ni nchi pekee ambayo mikoa yake zaidi ya 14 imekuwa ikipakana na nchi za jirani.
Kinana alisema  iwapo wananchi wa mikoa hiyo wakitumia fursa hiyo ya kupakana na nchi jirani kufanya biashara, kutawasaidia katika kuwaoongezea kipato.
“Ni lazima serikali ikaona namna njema ya kupunguza urasimu kwa wananchi kufanya biashara ya mipakani, ili waweze kuingia  katika nchi hizo jirani na kuuza bidhaa zao na kurudi,” alisema.
Alisema inashangaza kuona kuwa kunakuwa na urasimu wa wananchi kupeleka bidhaa zao nje ya nchi hizo.
“Mtu akitaka kuuza nje kitu anaambiwa hapana ni lazima kuuza humu humu ndani, sasa Kenya bei ni nzuri, mnamkataza asiende kuuza kwa kuwa hana kibali cha kusafiria kwanini?
«Huu ni urasimu na hata ningekuwa ni mimi, ningeuza bidhaa yangu hata mbinguni kama bei inakuwa nzuri huko kuliko hapa,» alisema Kinana .
Kinana alisema kumekuwa na ushuru ambao pia unachangia wananchi walio mipakani kushindwa kuuza bidhaa zao nje za nchi wanazopakana nazo.
Alisema ni vyema sasa kukawa na urahisi wa Watanzania kuuza bidhaa zao nje ya nchi kwa kuwaandalia utaratibu wezeshi wa kufanya hivyo.
Kinana alisema hivi sasa serikali haifanya biashara, hivyo ni kazi yake kuweka utaratibu  kwa wananchi kufanya biashara.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru