Wednesday, 11 March 2015

Kesi za albino kupewa umuhimu-Jaji Chande


NA FURAHA OMARY
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande, amesema mahakama itazipa kipaumbele kesi za mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) na mauaji ya vikongwe si tu kwa kiwango cha Mahakama Kuu, bali hadi Mahakama ya Rufani.
Amesema mauaji ya watu hao yanagusa kila Mtanzania na ni uhalifu wa hali ya juu na pia kuvunja haki za watu wengine.
Jaji Mkuu Chande aliyasema hayo jana mjini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Jaji Kiongozi Shaaban Lila, kuwaapisha manaibu wasajili 43.
“Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanagusa kila Mtanzania, ni uhalifu wa hali ya juu na ni kuvunja haki za wenzetu.
“Kila taasisi, idara na kila Mtanzania aguswe na mauaji haya kwa kuwa hayakubaliki,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema mahakama katika miaka michache iliyopita, ilikuwa na kesi zaidi ya 90 za mauaji ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe.
“Hivi karibuni nilifanya ziara mkoani Tabora, ambapo zipo kesi mbili zimepangwa kusikilizwa, huku Mwanza kukiwa na kesi tatu, moja imepangwa kusikilizwa na nyingine imemalizika,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema mahakama itazipa kipaumbele kesi hizo si tu kwa kiwango cha Mahakama Kuu, bali hadi Mahakama ya Rufani.
Alitoa wito kwa vyombo vyote kufanya kazi zao kwa bidii ili wahalifu wagundulike na kufikishwa mahakamani na ushahidi upatikane kwa mashahidi kutoa ushirikiano kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na sio kujificha.
Jaji Mkuu alisema kwa upande wao, mahakama wapo tayari kushughulikia kesi hizo kwa haraka.
Akizungumzia hafla ya kuapishwa kwa manaibu wasajili hao, Jaji Mkuu alisema uteuzi wa manaibu wasajili hao, wakiwemo waandamizi wawili, unafanywa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Jaji Mkuu alisema uteuzi huo unahitimisha muundo mpya wa mahakama na kwamba, manaibu wasajili hao wameshapewa majukumu mapya.
Alisema manaibu wasajili hao kazi yao ni kuratibu na kusaidia kwenye uendeshaji wa kesi.
Jaji Mkuu alitoa mfano wa kazi za manaibu wasajili hao kuwa ni kuandaa kalenda za kesi, kutayarisha nakala za hukumu na kwamba, wana mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza kesi za mauaji wakisaidiana na majaji.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, manaibu wasajili hao kusaidiana na majaji kusikiliza kesi za mauaji kutasaidia mashauri hayo kusikilizwa haraka.
Alisema Watanzania wategemee kupata huduma bora kutoka mahakamani kutokana na muundo mpya wa mahakama, ambao umetenganisha kazi za kihakimu, kiusajili na kiutendaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru