Tuesday 3 March 2015

Vijiji 244 kupata umeme Mbeya




WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda
 NA MWANDISHI WETU, MBEYA.
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema serikali itatumia sh. bilioni 55 kuvipatia umeme vijiji 244 vya mkoa wa Mbeya, kupitia Miradi ya Umeme Vijijini (REA).
Alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mbeya, waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara yake ya siku saba kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya.

“Nimeambiwa kuwa katika mwaka 2014/15, jumla ya vijiji 244 vitapatiwa umeme kupitia REA. Vijiji hivyo ni kama ifuatavyo: Chunya viko 13, Mbeya ni 32, Mbarali (56), Mbozi (14), Momba (15), Kyela (30), Ileje (18) na Rungwe (66) na jumla ya sh. bilioni 55 zitatumika kwa madhumuni hayo,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kusimamia suala la usambazaji wa umeme vijijini na kukamilisha awamu ya kwanza ya miradi ya umeme vijijini katika vijiji 17 vya mkoa huo.

“Nimeelezwa kuwa miradi hiyo iliyogharamu ya sh. billioni 7.6 katika vijiji 17 imekamilika kwa asilimia 100. Katika  Halmashauri ya Mbeya kuna vijiji vitano, Mbozi vijiji vinne, Chunya vijiji sita na Rungwe vijiji viwili na imeunganisha wateja 650,” alisema.

Alisema taarifa zinaonyesha kuwa vijiji vilivyopangwa kupata umeme wa REA mwaka 2015/2016 ni 51 na kwamba hivi sasa ujenzi wa njia kubwa ya umeme wa 11Kv na 33Kv unaendelea.
Aliwahimiza viongozi wa mkoa huo kuongeza jitihada za kusambaza umeme kwa kuwa mahitaji ya umeme ni makubwa kwa wananchi wengi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru