Tuesday, 17 March 2015

Chilolo awakumbuka wazee


MBUNGE wa Viti Maalumu Diana Chilolo, (CCM), amehoji mkakati wa serikali kuwasaidia wazee wasiojiweza walioko kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Diana alihoji hatua hiyo bungeni mjini hapa jana  alipokuwa akiuliza swali la nyongeza. Mbunge huyo  alitaka kujua ni lini serikali itaanza kuwalipa pesheni wazee wote nchini.
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, aliitaka jamii kuwasaidia wazee na kuwaondoa kwenye mazingira ya kuzurura.
Aidha, alizataka halmashauri nchini kuchukua hatua mahsusi kuhusu suala hilo na kutoa mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambalo liliwarudisha kwao wazee ombaomba.
Kuhusu pensheni,  Mahanga alisema hatua inayofuata ni kukamilisha rasimu ya mpango wa pensheni kwa kuzingatia uzoefu wa nchi zingine.
Alisema kunahitajika ushirikishwaji wa wadau wakiwemo Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha na kuwakilisha mpango wa pensheni katika vyombo vya uamuzi.
“Rasimu ya mpango wa pensheni kwa wazee wote imeandaliwa na ziara za mafunzo zimefanyika katika nchi mbalimbali,” alisema
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Kenya, Uganda, Mauritius, India, Thailand, China na Indonesia.
Hata hivyo, alisema lengo la ziara hizo zilizohusisha wabunge lilikuwa  kujifunza na kupata uzoefu wa nchi katika kuendesha mipango ya pensheni kwa wazee.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru