Na Michael Katona,
Njombe
KAZI ya uandikishaji wa
daftari ya kudumu la wapigakura kwa Mfumo wa Kielektroniki (BVR) katika mkoa wa
Njombe, limeanza rasmi katika kata za Mjimwema, Yakobi na Kifanya.
Hata hivyo, uandikishaji
huo umeanza kwa kulalamikiwa na wananchi kwamba unasuasua na kusababisha
wananchi wachelewe kwenye vituo, kutokana na mtu mmoja kutumia muda mrefu
kujiandikisha.
Mwandishi wa habari hii
alitembelea kata ya Mjimwema, katika vituo vya Melinze, Mjimwema, NJOSS, Mpechi
na Joshoni na kushuhudia msongamano wa wananchi waliopanga foleni
kujiandikisha.
Pia alishuhudia
mwananchi mmoja akitumia dakika 20 kuandikishwa, jambo ambalo lililalamikiwa na wananchi.
"Nipo hapa kwa muda mrefu katika kituo cha Melinze. Nimesimama toka saa 12 alfajiri nikiwahi labda nitaweza kujiandikisha mapema, lakini nilipomwuliza mtaalamu, alisema picha ninayopigwa ni lazima iende makao makuu Dar es Salaam halafu ndiyo kitambulisho kitoke," alisema Maria Sanga mkazi wa Melinze.
Robert Mkongwa, mkazi
wa mtaa wa Melenzi, akiwa amejiandikisha alisema ameshuhudia kazi hiyo ikicheleweshwa
na tatizo la vidole vyake kukataa kutambuliwa kwenye mashine kisha kurudia
zaidi ya mara tatu.
"Kilichonikuta ni uzoefu wa kuchukua taarifa zangu uandikaji ulikuwa taratibu, alama za vitole ziligoma. Nimerudia mara tatu ndiyo zikakubali. Nimetumia zaidi ya dakika 20 nikiwa ndani mpaka kukamilika na kupata kitambulisho," alisema Mkongwa
Uchunguzi umeonyesha
kuwa uandikishaji wa wananchi katika hilo umekuwa ukichukua dakika nyingi baina
ya watu watano kitu ambacho kimekuwa kikilalamikiwa na wananchi.
Kutokana na hali hiyo
wengine wamekuwa wakiondoka na kupeana
namba za simu kwa ajili ya kupata taarifa kama foleni imesogea ili aweze kurudi
kujiandikisha.
"Mimi nadhani hii kazi itakuwa na changamoto nyingi kwa hapa Njombe. Wataalamu wanaosimamia hii mitambo kwa ajili ya uandikishaji naona wengi hawana utaalamu wa kutosha, maana wamekuwa wakitumia muda mrefu kwa mtu mmoja," alilalamika Said Husein mkazi wa Joshoni.
Akizungumza juzi kabla
ya uandikishaji haujaanza, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Njombe, Hilmar Danda,
alisema mashine 250 zimesambazwa kwa kazi hiyo huku akiahidi kutojitokeza usumbufu wa
msongamano kwa kuwa kila baada ya dakika
tano mtu mmoja angekuwa ameshajiandikisha.
"Zile changamoto zilizojitokeza kule Makambako, tume imejipanga na kuzitatua. Iwapo mashine moja ingeleta dosari, tatizo hilo tumejipanga kulikabili," alisema Danda.
Mwandishi pia alipita
katika vituo vya Mpechi na NJOSS na Mjimwema na kukuta misururu mirefu kwa
ajili ya kujiandikisha, ambapo baadhi ya wananchi walilalamikia hali ya
kuchelewa kujiandikisha.
"Nipo hapa tangu saa 11
alfajiri kwa ajili ya kuwahi kujiandikisha, lakini huwezi amini mtu akiingia
ndani ya kituo anachukua zaidi ya dakika 20 hadi anapotoka. Hii hali naona inaleta kero sana," alisema Janeth
Mligo mkazi wa NJOSS.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru