Tuesday, 17 March 2015

Binti wa Nkurumah kuizindua ACT


NA MARIAM MZIWANDA
MTOTO wa Rais wa Kwanza wa Ghana, Dk. Kwame Nkurumah, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha CPP, Samia Nkrumah, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa chama cha ACT-Tanzania.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Machi 27-29, mwaka huu, jijini Dar es Salaam ambapo pia mkutano mkuu wa kwanza wa chama hicho utafanyika.
Samia, ambaye ameandika historia ya kuwa mwenyekiti wa kwanza mwanamke mwenye uwezo wa kuongoza chama kikubwa cha siasa nchini Ghana, atazungumza na wafuasi wa ACT na baadaye kukizindua rasmi.
Kabla ya uzinduzi huo, ACT itafanya mkutano mkuu wake ambapo ajenda kuu itakuwa kuwapata viongozi wa kitaifa, wakiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na manaibu wake.
Habari za kuaminika zinasema mbali na Samia, uzinduzi huo pia utahudhuriwa na mmoja wa marais wastaafu nchini pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama na wanasiasa.
Pia watakuwepo mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini, mashirika yasiyo ya kiserikali na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya ACT, kiu ya Watanzania kuwafahamu wanasiasa mahiri na maarufu waliopo nyuma, itakatwa kwenye mkutano huo.
“Maandalizi yote yamekamilika na hapa ndio vigogo wote ambao wapo na ACT lakini hawajajitanga ndio itajulikana. Mengi yamesemwa kuhusiana na chama hiki ila muda wa kuweka mambo hadharani ndio umewadia,” kimesema chanzo hicho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru