NA
LILIAN JOEL, ARUSHA
GARI
la Kampuni ya Kitalii ya Wengert Windrose, linashikiliwa na polisi kwa tuhuma
za kukutwa likiwa limepakiza shehena ya magunia 11 ya bangi.
Gari
hilo namba T 695 ARR aina ya Toyota Land Cruiser, likiendeshwa na Frank Faustine,
lilikamatwa eneo la Ranch wilayani Longido.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema gari hilo lilikamatwa saa
5:00 usiku na kwamba, bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwenda Kenya.
Juzi,
wabunge waliibana serikali wakitaka kuwekwa kwa sheria kali ili kudhibiti wimbi
la uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya nchini.
Wakichangia
Muswada wa Sheria ya Dawa za Kulevya,
wabunge walipendekeza kuwepo kwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa hadharani kwa
watakaotiwa hatiani.
Hata
hivyo, akiwasilisha muswada huo bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, alisema ili kuiongezea ukali sheria hiyo,
adhabu kwa watakaokutwa wakitumia au kufadhili dawa za kulevya zimeongezwa na
kuwa kali zaidi.
Alisema
kifungu cha 12 cha Sheria iliyopo, adhabu ya kujihusisha na kilimo cha mimea ya
dawa za kulevya (mfano bangi), inapendekezwa kuwa adhabu yake iwe faini
isiyopungua sh. milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka 30 au vyote kwa
pamoja.
Jenista alisema kosa la kufadhili biashara ya dawa za kulevya, kwa sasa adhabu
yake ni faini ya sh. milioni 10 wakati kwenye sheria inayopendekezwa, adhabu ni
faini ya sh. bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka 30.
“Kwa makosa ya kusafirisha na kufanya biashara ya dawa za kulevya, sheria ya sasa imetoa adhabu ya faini au kifungo cha maisha wakati katika sheria inayopendekezwa, adhabu inayowekwa ni kifungo cha maisha peke yake hivyo, kuondoa uwezekano wa wahalifu kupewa adhabu ya faini ambayo hulipa bila shida yoyote,” alisema.
Alisema sheria inayopendekezwa imeweka adhabu kali zaidi kwa watakaowashawishi
au kuwahusisha watoto kujiingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya
na inapendekeza adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 kwa kosa hilo,
tofauti na sheria ya sasa ambayo ipo katika eneo hilo.
Tayari
wabunge wamepitisha muswada huo na kinachosubiriwa ni kutiwa saini na Rais ili
kuwa sheria kamili.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru