MSAFARA wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, juzi ulilazimika kusimama kwa dakika kadhaa baada ya wakazi wa baadhi ya vijiji vya Jimbo la Chemba, kuusimamisha.
Kusimama kwa msafara huo kulitokana na wakazi wa vijiji hivyo kusimama barabarani wakiwa na mabango yanayoelezea kilio cha kukosekana kwa maji.
Msafara huo wa Kinana ulikumbana na kadhia hiyo, ulipofika
katika vijiji vya Songoro, Goima, Itolwa, Mrijo na Jenjelusi, maeneo ambayo wananchi wake wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la maji kwa muda mrefu.
Kinana hakuwa amepangiwa kusimama katika maeneo hayo, lakini kila alipowaona wananchi wanataka kuzungumza naye, alilazimika kusimama.
Katika vijiji vyote hivyo, Kinana alilazimika kusikiliza shida za wananchi huku katika baadhi ya maeneo, akiwaagiza watendaji kuyashughulikia.
Katibu Mkuu huyo alikiri kuwa sehemu kubwa ya Chemba inakabiliwa na tatizo la maji na akataka juhudi za makusudi zichukuliwe ili kuwanusuru wananchi wake, ambao wanapata maji kwa gharama kubwa.
Aliwaahidi wananchi hao kuwa, atafuatilia suala hilo kwa Waziri wa Maji, ili afike huko na kujionea hali halisi na kutafuta njia ya kupunguza kero hiyo na ikiwezekana kumalizika kabisa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, alisema tatizo la maji katika jimbo lake linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fedha kutoka serikali kuu.
Alisema endapo fedha zingekuwa zikitolewa kwa wakati, miradi mingi ikiwemo ya maji ingekuwa imekamilika muda mrefu uliopita.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu hata huu mradi wa Ntomoko, ambao una sifa na historia ya kipekee kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alishiriki ujenzi wake, fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni moja tu kati ya bilioni tatu zilizoahidiwa,» alisema.
Alisema mradi huo wa Ntomoko endapo utakamilika, utakuwa mkombozi mkubwa wa upatikanaji wa maji katika mji wa Kondoa, ikiwemo wilaya ya Chemba.
Thursday, 12 March 2015
Wanavijiji wasimamisha msafara wa Kinana
08:13
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru