Tuesday 17 March 2015

Shekifu alia na tatizo la maji


 MBUNGE wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu, amelalamikia tatizo la maji mkoa wa Tanga na kuilaumu serikali kwa kutoa ahadi za mara kwa mara huku ikishindwa kuzitekeleza.
Akiuliza swali bungeni mjini hapa jana, Shekifu alisema kwa muda mrefu serikali iliahidi kupeleka maji katika wilaya ya Muheza lakini haijatimiza.
Aidha, Shekifu alitaka kuhakikishiwa kama kuna fungu lolote lililotengwa kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maji katika wilaya hiyo kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha.
“Serikali inatamka nini katika ahadi zake ambazo hazionyeshi kutekelezwa,” alihoji.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Al-Shaymaa Kwegyir, lililoulizwa kwa niaba yake na Shekifu, alitaka kujua ni kwa nini hadi sasa hakuna juhudi za makusudi za kuhakikisha maji yanapatikana kutoka Mto Zigi ili kumaliza tatizo sugu la maji mkoani Tanga, hususan Muheza.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji, Amosi Makalla, aliwaomba wabunge kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo pale muda utakapofika ili fedha za kutosha zitengwe kwenye miradi mbalimbali mkoani Tanga.
Alisema miradi yote iliyo kwenye ahadi ya serikali itafanyiwa kazi na kukamilishwa kulingana na uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.
Kwa mujibu wa Makalla, ili kutatua tatizo la maji katika mji wa Muheza, serikali imeandaa mpango wa muda mrefu wa kuboresha huduma hiyo kwa kutoa maji kutoka Mto Zigi hadi Muheza mjini na vitongoji vyake.
Makalla, alisema wizara kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mkoa wa Tanga ilimwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru