Tuesday, 10 March 2015

Kamati ya Bunge yataka mradi umalizike kwa wakati

NA WILLIAM SHECHAMBO, Morogoro

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo, na Maji, imesisitiza kukamilika kwa mradi wa maji wa Ubena Zomozi, ulioko Chalinze mkoani Pwani katika muda uliopangwa.

Mwenyekiti, Prof. Msolwa (Mwenye shati jeupe)
Imesema hatua hiyo itawapa unafuu wananchi wa vijiji kadhaa vya wilaya za Bagamoyo na baadhi ya maeneo ya Morogoro, kutokana na kukumbwa na shida ya maji kwa kipindi kirefu.

Akitoa maelekezo hayo kwa mkandarasi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Peter Msolwa, alisema anazo taarifa kuwa Wizara ya Maji imetoa mahitaji yote kwa miradi inayoendelea na kwamba hakuna sababu ya kuchelewa kuikamilisha.

Alisema wananchi wanahitaji kunufaika na matunda ya serikali yao ya awamu ya nne, kwa kuona huduma zote muhimu wanazipata mahali walipo.

Profesa Msolwa aliyeambatana na wajumbe wengine wa kamati yake, alisema licha ya changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa fedha, miradi ya huduma muhimu ikiwemo maji, inatakiwa kukamilika kwa muda uliopangwa kwa ubora unaotakiwa kwa hali yoyote ile.

Akielezea maendeleo ya mradi huo na muda wanaoamini kuukamilisha, Mhandisi Mkazi, Osama Kamel, alisema kwa kuwa Wizara ya Maji imewapatia mahitaji yote, watamaliza mwanzoni mwa Julai, mwaka huu.

Alisema mahitaji hayo ni miundombinu na vitendea kazi, lakini wanayo changamoto ya fedha, ambazo mara kwa mara zinachelewa kiwafikia, jambo ambalo hata hivyo sio kizuizi kwao kumaliza kazi.

"Tumepewa na wizara pampu za maji zenye uwezo mkubwa tu, jenereta za dharura na vitendea kazi vingine muhimu, hivyo lazima Julai tumalize huu mradi na kuukabidhi.

Aliongeza kuwa, "Fedha kweli ni tatizo, lakini halituzuii kufanya kazi na kukamilisha kama tulivyoahidi kwani kuna benki nyingi tu tunafanya nazo kazi, hivyo serikali iondoe shaka sisi ni wazawa.

Kwa upande wao, wakazi wa Kata ya Kidugalo, mkoani Morogoro, ambao pia watanufaika na mradi huo, waliiambia kamati ya bunge kuwa maji hayo yatakuwa mkombozi kwao kutokana na uwepo wa tatizo hilo sugu.

Mradi huo wa Ubena zomozi, utatumia maji ya mto Wami, kwa ajili ya kuwahudumia wananchi hao, ambapo kila kijiji kitajengewa kisima cha ujazo kulingana na uhitaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru