Tuesday, 17 March 2015

Vigogo wanne wa shule kizimbani kwa rushwa


NA MWANDISHI WETU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Nachingwea, imepawandisha kizimbani wajumbe wa kamati ya shule kwa tuhuma za rushwa.
Wajumbe hao walipandishwa kizimbani Machi 11, mwaka huu, katika Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea, wakishitakiwa kufanya ununuzi hewa ya vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya sh. milioni 1.3 kwa ajili ya Shule ya Msingi Farm Eight.
Kesi hiyo namba CC20/2015, ilifunguliwa Machi 11, mwaka huu, ambapo washitakiwa hao ni Hamza Chidoli (Mwalimu Mkuu) na Liberatus Mwaya (Mwalimu Mkuu Msaidizi). 
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya shule, Somoe Nyagali na mfanyabiashara mzabuni, Jahida Kalinga, ambao walinunua vifaa hewa walivyodai kuwa ni mbao, kokoto na mchanga. 
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa TAKUKURU wilayani Nachingwea, Moses Oguda, washitakiwa walisomewa mashtaka na Wakili Dismas Mganyizi.
“Makosa wanayoshtakiwa nayo ni kuisababishia hasara mamlaka ya Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kinyume cha kifungu cha 57 jedwali la kwanza aya ya 10 ya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 ya mwaka 2002,” inaeleza taarifa hiyo.  
Kosa la pili ni kutumia nyaraka za kughushi kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. 
Kosa la tatu ni kughushi nyaraka kinyume cha kifungu cha 333, 33(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyorejewa mwaka 2002, ambapo kosa la nne ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Katika kosa la tano, washitakiwa hao wanadaiwa kula njama kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya 2007.
Washitakiwa walikana tuhuma hizo na wapo nje kwa dhamana hadi Aprili 13, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru