Thursday, 5 March 2015

Gurumo: Aulizwe Rugemalira ndio amenipa fedhaNA WAANDISHI WETU
MNIKULU katika Ofisi ya Rais Ikulu, Shaaban Gurumo, amesema hajui fedha alizopewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira zilikuwa ni za nini ndio maana alizitumia atakavyo.
Aidha, ametaka watu wanaohoji kuhusu fedha hizo, wamkabili Rugemalira kwa kuwa ndiye anayejua sababu za kumpatia.
Alisenma hawezi kujua Rugemalira alimpa fedha kwa lengo gani, kwa kuwa hicho ni kiasi kidogo na cha kawaida kwake kulingana na fedha alizonazo, hivyo hata matumzi yake yalikuwa ni ya kawaida.

“Mimi nina pesa zangu zaidi ya hizo nilizoingiziwa na Rugemalira ambazo ni kiasi cha kawaida kutokana na uhusiano wetu wa kijamii hivyo, nilitumia nitakavyo bila kujua ni za nini kwa kuwa ni zangu na nilitoa mfuko huu na huu kadri mitakavyo na kufanya matumizi,” alisema.

Gurumo alisema hayo mbele ya Baraza la Maadili ya Utumishi wa Viongozi wa Umma wakati akihojiwa na baraza hilo kuhusu manufaa aliyoyapata kutokana na mgao wa uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta escrow.
Akisomewa tuhuma zinazomkabili na Mwanasheria wa baraza hilo Hassan Mayunga, alimtaka Gurumo kujitetea kwa nini akiwa kiongozi wa umma asichukuliwe hatua kutokana na kunufaika na kujihusisha na mgongano wa maslahi.
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kupokea zaidi ya sh. milioni 80 kutoka kampuni ya VIP ni ukiukwaji wa fungu la 6(e) la sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Aidha, anadaiwa kutumia wadhifa wake kujipatia manufaa ya kifedha na fadhila za kiuchumi kwa maslahi binafsi.
Naye shahidi wa upande wa mlalamikaji, ambaye ni Ofisa Uchunguzi wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Bazilio Mwanakatwe, alisema uchunguzi uliotokana na taarifa za viongozi wa umma kupokea fedha kutoka kwa Rugemalira  ulibaini Gurumo kuhusika kupokea sh. milioni 80.8.
Alisema mlalamikiwa alipokea fedha hizo kupitia akaunti namba 00110102645401 Benki ya Mkombozi tawi la St. Joseph, Dar es Salaam.

“Mlalamikiwa alikiri katika mahojiano na Kamati ya Uchunguzi kuwa amepokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, akiwa kiongozi wa umma anakatazwa kupokea fadhila za kiuchumi au zawadi zaidi ya 50,000 hivyo, kwa majukumu aliyonayo ana fursa ya kujinufaisha kiuchumi na kisiasa na fedha hizo,” alisema.

Gurumo alijitetea kuwa kutokana na majukumu yake ambapo ni Kiongozi Mkuu wa Watumishi wa Idara ya Ndani ya Ikulu, msimamizi wa uundwaji na matengenezo ya makazi ya rais, majengo ya ofisi za rais nchini.
Alisema pia ndiye mpokeaji wa wageni wa Ikulu wakiwemo mabalozi, marafiki na kuandaa tafrija na dhifa zote za Rais hivyo, hajawahi kuwa na maslahi au fadhila za kiuchumi kutoka kwa  Rugemalira kwa nafasi ya kikazi.
Alidai kufahamiana na Rugemalira takribani miaka 10 iliyopita akiwa ameunganishwa na daktari wa familia yake, Fred Limbanga.

“Rugemalira ni rafiki yangu wa kijamii zaidi ya miaka kumi na alinitaka nifungue akaunti Mkumbozi nikafanya hivyo na akaniwekea kiasi hicho cha fedha bila kujua ni za nini na sikuhoji,” alisema

Gurumo alisema kutokana na kutokuwa na shaka na fedha hizo ni moja ya kipato alichokiwakilisha katika ripoti ya rasilimali na mapato yake ya kila mwaka kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Nilishangazwa na taarifa nilizozisikia kwa mara ya kwanza nikiwa njiani kutoka Afrika Kusini watu wakizoza na kubwawaja kuwa amepokea milioni 800 kutoka kwa Rugemalira,” alisema na kuongeza: Naliomba baraza hili lipokee lalamiko langu rasmi kwa waliosema kuwa nimepokea sh. milioni 800 wakiwa viongozi wa umma kama walifanya makusudi wachukuliwe hatua”.

Mwanasheria wa Baraza hilo Getrude Cyriacus, alisema Gurumo alikuwa akitumia fedha hizo zilizoingizwa Februari 5 na 9, mwaka jana, ambapo alitoa Machi 11, mwaka jana, alitoa sh. Milioni 15, na baadaye sh. Milioni 40 na Mei 8 alitoa sh. milioni 8.
Aidha, Juni 12, mwaka jana, alitoa milioni 9, Julai 28 milioni 3.5, Agosti 13, alitoa sh. milioni 5 na hadi kufikia Desemba 18, 2014 alikuwa ametumia sh. milioni 77 zilitolewa katika akaunti yake.
Getrude: Unasema hujui fedha ni za nini, uliwezaje kufanya matumizi
Gurumo: Sikuomba na sifahamu fedha hizo ni za nini ingawa baada ya kuzipokea nilichokiwaza ni kuwa nimepewa kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa wangu ambaye Rugemalira anamfahamu”.
Getrude: Sasa kama fedha hizi sio zawadi, ni mshahara wako ama posho. Ulipewa kwa manufaa gani?
Gurumo: Kwani wewe hujawahi kupewa tu fedha na mtu bila sababu? Kama sivyo basi nenda kamuulize Rugemalira nadhani ndiye anayejua  kuhusu hili. Hakuna mtu ambaye hajawahi kupewa pesa.
Jaji Mstaafu wa Baraza hilo, Hamisi Msumi aliahirisha shauri hilo hadi Machi 13, mwaka huu,  ambapo uamuzi utatolewa baada ya mamlaka husika kupitia majumuisho kulingana na ushahidi wa pande zote mbele.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru