NA WAANDISHI WETU
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es
Salaam, imetupilia mbali kesi ya msingi iliyokuwa imefunguliwa na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), dhidi ya chama hicho.
Kutokana na kutupiliwa mbali kwa kesi
hiyo, uongozi wa CHADEMA, ulitangaza jana kumtimua uanachama Zitto na kumvua nyadhifa zake zote
za kichama.
Uamuzi wa mahakama ulitolewa jana na Jaji
Richard Mziray, baada ya kukubaliana na moja ya mapingamizi ya awali
yaliyowasilishwa na mawakili wa CHADEMA, kupinga kesi hiyo.
Zitto alifungua kesi hiyo namba moja ya
mwaka jana, dhidi ya bodi ya wadhamini ya chama hicho na Katibu Mkuu wa
CHADEMA.
Katika shauri hilo, alikuwa anaiomba
mahakama iamuru Kamati Kuu ya CHADEMA na chombo chochote cha chama hicho,
kutojadili na kuchukua uamuzi kuhusu uanachama wake hadi rufani yake
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na baraza kuu la chama hicho.
Pia alikuwa anaiomba mahakama imwamuru
katibu mkuu huyo, ampatie mwenendo wa kikao cha Novemba 22, mwaka jana, cha
baraza kuu ambacho kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake zote za kichama.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Mziray
alikubaliana na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawakili wa CHADEMA na
kuitupilia mbali kesi hiyo, kwa kuwa ilifunguliwa bila ya kufuata utaratibu wa
kisheria.
Jopo la mawakili wa CHADEMA, likiongozwa
na Tundu Lissu, akishirikiana na Peter Kibatala na John Mallya, waliwaslisha
mapingamizi ya awali matano kupinga shauri hilo.
Moja ya mapingamizi hayo, yalikuwa ni
kwamba kesi kufunguliwa Mahakama Kuu haikuwa jambo sahihi kwa kuwa ingepaswa
kufunguliwa mahakama ya wilaya au hakimu mkazi kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo
wa Kesi za Madai.
Pia, walidai kesi hiyo ilikosewa
kufunguliwa Mahakama Kuu, Masijala Kuu badala ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam.
Katika uamuzi wake, Jaji Mziray
alikubaliana na mawakili wa CHADEMA na kutupilia mbali kesi hiyo na kuamuru
chama hicho kulipwa gharama zote za kuendeshea shauri hilo.
Wakizungumza baada ya kutolewa kwa uamuzi
huo, Kibatala alisema akiwa wakili, alitumwa mahakamani hapo na CHADEMA, hivyo
amemaliza kazi yake na atakabidhi nakala ya hukumu kwa chama.
Kwa upande wake, Lissu alisema kwa mujibu
wa katiba ya CHADEMA, ni marufuku kupeleka mambo ya chama mahakamani kwa kuwa
unajifukuzisha uanachama mwenyewe.
Atangazwa kutemwa rasmi
Baada ya mahakama kutoa uamuzi huo,
CHADEMA ilifanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama
hicho, Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo Mwanasheria wa chama hicho, Lissu
alitangaza kumfukuza uanachama Zitto.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida
Mashariki, alisema katika kufungua kesi
hiyo, Zitto alikiuka utaratibu kwa kuwa hakupaswa kufungua Mahakama Kuu ya
Tanzania bali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au Masijala ya Wilaya ya Mahakama
Kuu.
“Katiba ya CHADEMA inatamka wazi hatua anazochukuliwa mwanachama baada ya kuikiuka, ambazo ni kwamba haruhusiwi kuchukua hatua za kukishitaki chama mahakamani.
“Zitto alikishitaki chama mahakamani, hivyo alipuuza katiba ya chama. Kutokana na hatua hiyo, CHADEMA imemfukuza rasmi uanachama kuanzia leo hii (jana),” alisema Lissu.
Alisema
chama hicho kilikwishamfukuza uanachama Zitto muda mrefu, lakini uamuzi
ule ulikuwa wa kisiasa.
Alisema baada ya Zitto kukimbilia
mahakamani na mahakama kufutilia mbali pingamizi lake, chama kimemfukuza na
kumvua nyadhifa zake zote.
“Kuanzia leo (jana) Zitto si mwanachama wa CHADEMA na tutawasilisha taarifa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuieleza kuwa yule aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa dhamana ya CHADEMA, Zitto Kabwe, si mwanachama tena wa chama hicho,” alibainisha mwanasheria huyo.
Alisema Zitto alitabiri mwenyewe kupitia
vyombo vya habari, ambapo CHADEMA
ilimnukuu akisema kuwa hatima yake ndani ya chama itakuwa ni Machi, mwaka huu.
“Alitabiri mwenyewe kuwa hatima yake itakuwa mwezi Machi, mwaka huu. Hatimaye imetimia leo (jana). Kesi hamna na uanachama hamna. Umekoma rasmi,” alisema.
Akizungumzia juu ya nguvu ya Zitto na
umuhimu wake ndani ya CHADEMA, hususan
kutokana na kujizolea umaarufu zaidi kupitia sakata la akaunti ya Tegeta
Escrow, Lissu alidai sauti ya Zitto katika sakata hilo ilitokana na uamuzi
uliokuwa unachukuliwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
anayoiongoza na si vinginevyo.
“Itakumbwa kuwa, wakati sakata la Escrow linajadiliwa bungeni, lilipingwa vikali kiasi cha Zitto kutaka kubwaga manyanga ili lisijadiliwe.
Lakini sauti yetu kama Ukawa ndiyo ilichochea suala hilo kujadiliwa na watuhumuwa kuchukuliwa hatua. Yeye mwenyewe alikuwa na tuhuma za kuchota fedha. Hivyo alikuwa hana sauti. Sifa ile ya Escrow haiwezi kumfanya Zitto aonekane maarufu kama Zitto bali ni kwa kamati nzima ya PAC,” alisema Lissu.
Lissu alimshambulia Zitto kwa kudai
kwamba kama anategemea kupata sifa kwa wananchi kupitia sakata la Escrow, imekula kwake.
“Isitoshe katika uongozi wake, CHADEMA ilipoteza nguvu Kigoma Kaskazini, lakini baada ya uongozi kuchukua uamuzi wa kuwaondoa wale wote waliokuwa wanakisaliti chama, akiwemo yeye CHADEMA Kigoma imeanza kuimarika,” alisema.
Mwigamba: CHADEMA ni dhaifu
Katibu Mkuu wa Chama cha ATC, Samson
Mwigamba, alisema maamuzi yaliyochukuliwa na CHADEMA yanaonyesha udhaifu mkubwa
kisiasa.
Alisema viongozi wa chama hicho si
waelewa na kwamba uamuzi wa kumfukuza ulikuwa uchukuliwe na Kamati Kuu ya
CHADEMA na sio Lissu.
Hata hivyo, alisema hakuna haja kwa Zitto
kung’ang’ania CHADEMA, badala yake alimtaka ajiunge na ATC.
Zitto: Sivurugiki ng’o
Jitihada za kumtafuta Zitto kuzungumzia
uamuzi huo, hazikuweza kuzaa matunda hata alipotafutwa kupitia simu yake ya
kiganjani, ambayo muda mwingi ilikuwa imezimwa.
Hata hivyo, kupitia mtandao wake wa
kijamii, Zitto aliandika kuwa ameshangazwa kama suala la kashfa ya Escrow
lingepita kimya kimya.
Amesema kwa namna kazi hiyo
ilivyofanyika, waathirika wa kashfa hiyo wasingeweza kukaa kimya bila kujaribu
kumvuruga, lakini kwa bahati mbaya havurugiki.
Aliongeza kuwa kwa sasa anaendelea na
kazi zake za Kamati ya PAC kama kawaida na jana, walikutana na maofisa wa EWURA
kujadili masuala mbalimbali.
“Ningeshangaa kama Escrow ingepita kimya kimya bila waathirika kujaribu kunivuruga. Bahati mbaya sana sivurugiki, leo (jana) tumekutana na EWURA kukagua hesabu zao, kesho (leo) tutakutana na TANESCO kisha tutamalizia na mabilioni ya Uswisi,” alisema.
Hata hivyo, kuhusiana na kufukuzwa
uanachama na uamuzi wa mahakama, alisema hafahamu lolote kwa kuwa hakuwa na
wito wa mahakama.
Pia, alisema jaji anayesikiliza kesi
hiyo, Jaji John Utamwa, amehamishiwa mkoani Tabora na hakuna taarifa ya kuwepo
kwa jaji mpya mpaka sasa.
Aliongeza kuwa mwanasheria wake
anafuatilia suala hilo na baadaye watatoa tamko rasmi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru