NA SAMSON CHACHA,
TARIME
UKAMATWAJI wa malori
yanayosafirisha mizigo kwa njia ya magendo kutoka Kenya kwa kupitia mpaka Sirari
mkoani Mara, umezidi kushika kasi ambapo jana yalikamatwa matatu yaliyosheheni bidhaa
mbalimbali zikiwemo nondo na saruji.
Magari hayo
yalikamatwa kwa ushirikiano wa Maofisa wa Forodha wa kituo cha Sirari
wakishirikiana na wenzao wa kodi za ndani wilayani hapa.
Akizungumzia tukio
hilo, Meneja wa Forodha Mkoa wa Mara, Ben Usaje, alisema magari hayo ni fuso
mbili zenye namba T175 BEZ na T385BMQ mali ya Eliya Mangarama, mkazi
wa Bunda.
Lingine ni Toyota Hiace
namba T556 CLW mali ya Mwita Nyangi, mkazi wa Sirari ambayo yalikuwa
yamesheheni saruji, mabomba, nondo, viberiti na chumvi.
Usaje alisema mali
hizo zimeingizwa nchini kupitia njia za panya bila ya kulipiwa ushuru kwa nia
ya kukwepa kodi hivyo kuikosesha serikali mapato.
Alizitaja baadhi ya
njia zinazotumika kuwa ni mipaka ya Kogaja, Kubiterere na Sirari na kwamba,
magari na mali zote zimezuiwa hadi hapo wahusika watakapolipa kodi pamoja na
faini.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru