Wednesday, 11 March 2015

MAUAJI YA ALBINO


  •  Wapiga ramli 225  wanaswa na polisi

NA MWANDISHI WETU
JUHUDI za kukomesha matukio ya kihalifu ya kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino’, zimeanza kuzaa matunda baada ya Jeshi la Polisi kuwashikilia wapiga ramli 225.
Kushikiliwa kwa wapiga ramli hao kunatokana na operesheni inayoendeshwa na polisi ya kupambana na vitendo vya kikatili ili kuhakikisha matukio hayo hayaendelei kutokea.
Taarifa iliyotolewa jana mjini Dar es Salaam na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, ilisema wapiga ramli hao walikamatwa kwenye mikoa ya Tabora, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Kagera, Katavi na Rukwa.
Alisema kati ya hao, 97 wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kukutwa na vifaa vya uganga.
Advera alisema mbali na vifaa hivyo, pia walikutwa na nyara za serikali kama vile ngozi ya kenge, meno ya ngiri, mikia ya tumbili, miguu ya ndege, mikia ya nyumbu, ngozi ya simba, ngozi ya fisi na ngozi ya digidigi.
Hata hivyo, alisema baadhi ya waganga hao walikuwa  wakifanya uganga bila vibali.
Advera alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya operesheni kali katika mikoa yote ili kuhakikisha mtandao unaojihusisha na matukio hayo unakamatwa, wakiwemo waganga wa jadi na wapiga ramli chonganishi.
Alisema mauaji ya albino yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na imani potofu za kishirikina.
Advera alisema baadhi ya wananchi wanaamini imani za kishirikina zinaweza kuwasaidia kupata utajiri na mafanikio mengine kimaisha.
Aliwataka wananchi kuacha imani hizo ili matukio hayo yakomeshwe.
Aidha, aliwataka wananchi watoe taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na wanaoeneza imani potofu za kishirikina.
Advera alisema Jeshi la Polisi linawaomba wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, wanasiasa, wazee wa kimila, wanahabari na wananchi kwa ujumla, kuielimisha jamii kuachana na imani za kishirikina ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
UTSS YALAANI
Shirika la Under The Same Sun (UTSS), limelaani vikali kitendo cha kinyama cha kukatwa kiganja mtoto Baraka Cosmas Rusambo (6).
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa UTSS, Vicky Ntetema, ilisema katika tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Prisca Shaaban alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa mapanga kichwani.
Alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika Kijiji cha Kipeta, Kata ya Kiseta wilaya ya Sumbawanga Vijijini mkoani Rukwa, ambapo majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya.
Vicky alisema pamoja na hatua zilizochukuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali dhidi ya matukio hayo ya kinyama, bado matendo hayo  yanaendelea kutokea nchini.
Alisema wakati umefika sasa makundi mbalimbali katika jamii kushirikiana ili kutafuta ufumbuzi wa matukio hayo.
Vicky alipongeza kauli na ahadi alizozitoa Rais Jakaya Kikwete wakati akifanya mkutano na viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS),  kwamba serikali itafanya kila iwezalo ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya pamoja ya wadau kutafuta njia muafaka ya kukomesha mauaji hayo.
Alisema mkutano huo ulikubaliana kufanyiwa mapitio kwa sheria zinazohusu uchawi na waganga wa jadi.
Vicky aliwaomba wabunge wanaotoka kwenye maeneo yaliyoathirika na kadhia hiyo, kufanya kikao cha pamoja kujadili namna ya kutokomeza unyama huo na waliombe Bunge lijadili na kuielekeza serikali na vyombo vyake hatua na mbinu stahili za kuchukua.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru