Wednesday, 18 March 2015

Mabilioni kujenga barabara za juu


WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema ujenzi wa barabara za juu katika jiji la Dar es Salaam, utagharimu sh. bilioni 78.
Ujenzi huo wenye lengo la kupunguza msongamano wa magari huku serikali ya Japan ikichangia sh. bilioni 26 kusaidia ujenzi huo.

Akichangia majibu ya swali lililoelekezwa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Magufuli alisema tayari mchakato wa ujenzi huo umeanza.
Kauli hiyo ilitokana na maswali ya Mariam Kisangi (Viti Maalum –CCM), kuhoji mpango wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni pamoja na uwanja wa ndege wenye hadhi ya mji huo.
Awali, akijibu swali la msingi la Mariam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Charles Tizeba, alisema kuna mipango mizuri ya kuendeleza mji wa Kigamboni.
Hata hivyo, alisema mji mpya wa Kigamboni utakuwa ndani ya jiji la Dar es Salaam, ambako kuna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
“Kiwanja hiki kina uwezo wa kuhudumia ndege 30 kwa saa baada ya kukamilika kwa upanuzi wa miundombinu na ukarabati wa Awamu ya Pili. Kwa sasa tunahudumia ndege nane kwa saa ambazo ziko chini ya kiwango,” alisema Dk. Tizeba. 
Aliongeza kuwa mpango wa sasa ni kuendelea kukipanua kiwanja hicho kwa kujenga jengo jipyha la tatu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru