Wednesday 18 March 2015

Kinana awalipua viongozi UKAWA



  • Awaonya uchu wa madaraka utawamaliza
  • Ngome ya CHADEMA Karatu yagaragazwa

Na Mwandishi Wetu, Karatu
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema mwisho wa ndoa ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umekaribia.
Amesema muungano huo utabadilika jina na kuwa Ukiwa, ifikapo Oktoba, mwaka huu, wakati mgombea urais wa CCM pamoja na idadi kubwa ya wabunge wake watakapotangazwa washindi.
Alisema kelele nyingi zinazopigwa na viongozi wa UKAWA na mikakati lukuki wanayoizungumza katika kuhakikisha wanashika dola, ni sawa na ndoto za Abunuasi.
Kinana alisema mabadiliko hayo ya jina yanatokana na kelele nyingi pamoja na mikakati mingi wanayoizungumza ya kuchukua madaraka ya urais, jambo ambalo alilisema ni sawa na ndoto ya Abunuasi.
“Siku zote mikakati ya mtu ama chama hakielezi mikakati yake hadharani kama ilivyo kwa UKAWA, ambao wanazunguka na kueleza mambo ambayo kihalisia hayawezekani. 
“Upinzani haujaaminiwa vya kutosha na Watanzania katika kuongoza nchi, hivyo watakuwa na wakati mgumu kwa kuwa CCM bado inaaminiwa,” alisema Kinana.
Kuhusu UKAWA kuwa na mkakati wa kusimamisha mgombea mmoja wa urais, Kinana alisema bado una changamoto nyingi huku viongozi hao kila mmoja kuwa na uchu wa madaraka.
Kutokana na uchu huo wa madaraka, ambao umeanza kuvitikisa vyama hivyo, kwa sasa kila kimoja kimekuwa kikijipanga kutangaza mgombea wake, hivyo mkakati huo kugonga mwamba.
“Hawa jamaa wana uchu wa madaraka, suala la kusimamisha mgombea mmoja halipo. Tayari NCCR -Mageuzi wana mgombea urais, CHADEMA na CUF navyo vimetangaza kutaka kusimamisha wagombea wao, hapa kutazuka mgogoro mzito na watasambaratika kabla ya muda,” alisema.
Ngome Karatu yaanguka
Katika ziara yake wilayani Karatu, Kinana alivunja vunja ngome za CHADEMA na kuzoa wanachama zaidi ya 400, ambao walitangaza kujiunga na CCM.
Jimbo la Karatu ni moja ya ngome imara za CHADEMA, ambapo idadi kubwa ya wanachama waliohamia CCM walieleza kuchukizwa na sera mbovu za chama hicho.
Kinana aliwapokea wanachama hao wapya kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mazingira, ambao ndio uliokuwa ukihitimisha ziara yake wilayani hapa.
Emanuel Karato, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema amekuwa mfuasi wa CHADEMA kwa zaidi ya miaka 15, lakini amekuwa akikerwa na ubaguzi ulioota mizizi ndani ya chama hicho.
Alisema kitongoji cha Magesho wanachotoka wanachama hao, kinakabiliwa na kero nyingi, ikiwemo ubovu wa barabara, ukosefu wa zahanati, maji safi na salama na migogoro ya ardhi, lakini hakuna walichosaidiwa na viongozi ambao wengi ni wa CHADEMA.
Kinana aliwapongeza wanachama hao kwa kutambua kuwa CCM ndio inayojenga nchi na kuachana na propaganda za upinzani, ambao kazi kubwa ni kupiga kelele zisizo na tija.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru