Tuesday 3 March 2015

Ngeleja amlipua Zitto Kabwe Barazani




NA MARIAM MZIWANDA.
MBUNGE wa Sengerema, William Ngeleja, amemgeuzia kibao Zitto Kabwe kuwa ni mmoja kati ya watu walionufaika na fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.

Ngeleja, amemtaja Kabwe (Mbunge wa Kigoma Kaskazini), kuwa amejipatia zaidi ya sh. milioni 30 na hakuna mamlaka, likiwemo Bunge zilizochukua hatua dhidi yake.

Aliyasema hayo jana wakati akitoa utetezi wake mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo alikiri kupata fedha kiasi cha sh. milioni 40 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.

Hata hivyo, alikanusha kupokea fedha hizo kama fadhila za kiuchumi kinyume na fungu la 6 (f) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Ngeleja alisema kamwe hajawahi kuomba wala kupokea fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira na kwamba, alipewa msaada huo kama ilivyo kwa wabunge wengi nchini.

Alisema hakuna mbunge anayefanya kazi bila kuomba msaada kwa mashirika, taasisi na wadau wa maendeleo na kwamba, wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

"Baadhi ya misaada hiyo ni uwezeshaji wa vikundi na michango katika miradi ya maendeleo kwa wananchi ambayo haikutengewa fedha.

"Wabunge wengi wamekuwa wakipewa misaada kwa ajili ya maendeleo ya wapiga kura. Msaada wa Rugemalira hauna tofauti na wanayopewa wabunge na wafadhili wengine," alisema Ngeleja.

Aliongeza: "Hapa nina mifano michache na vielelezo vya ushahidi kuhusu namna ambavyo wabunge tumekuwa tukipewa misaada."

Alisema mfano na kielelezo cha kwanza ni wakati taarifa au hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Alisema taarifa hiyo ilihoji uhalali wa Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), na washirika wake, kupata msaada wa zaidi ya sh. 119,930,000 kutoka katika taasisi za umma, ambazo ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo ilitoa sh. milioni 12.2 na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambayo ilitoa sh. milioni 79, katika kipindi cha miezi mitatu yaani Desemba 10, 2012 na Machi 4, 2013.

Hata hivyo, alisema pamoja na hoja hizo kuwasilishwa bungeni, kamwe Bunge halikuwahi kumuita Zitto wala kumwajibisha kwa hilo.

Kielelezo kingine kilichowasilishwa na Ngeleja ni hoja zilizotolewa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, akimtuhumu Zitto kupokea msaada wa zaidi ya sh. milioni 30 kutoka kwa Kampuni ya PAP.

Zitto anatuhumiwa kupokea fedha hizo kati ya Machi 28 na Aprili 8, mwaka jana, ambazo ni kwa matumizi yake binafsi.

"Wakati akijua PAP inahusishwa na kadhia ya Escrow, Zitto alituhumiwa kujinufaisha na zaidi ya sh. milioni 30. Machi 28, alipokea sh. milioni sita, Aprili 3, alipokea dola 5,000 (zaidi ya sh. milioni saba, Aprili 8 alipokea sh.milioni 10 na siku hiyo hiyo alipokea tena sh. milioni 10," alidai Ngeleja.

Alisema pamoja na tuhuma hizo na kuwepo kwa vielelezo, Bunge limekaa kimya bila kuchukua hatua dhidi ya Zitto.

"Naomba nyaraka na vielelezo hivi vipokelewe kama sehemu ya maelezo ya utetezi wangu, na kutokana na maelezo hayo, nasisitiza msaada nilioupata kutoka kwa Rugemalira haukuwa fadhila za kiuchumi, ni msaada wa kawaida kama wapatavyo wabunge wengine," alisema.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Mkombozi, Februari 12, 2014, alipokea msaada wa fedha zaidi ya sh. milioni 40 kutoka kwa Rugemalira, kwa ajili ya kusaidia shughuli za kibunge.

"Msaada alionipa Rugemalira ni kupitia akaunti yake ya benki anayoimiliki ya VIP TZS Trust, iliyoko Benki ya Mkombozi. Sijapokea msaada kutoka VIP, ni wazi kwamba kisheria, kimantiki na hata kiuhalisia, VIP TZS TRUST ni tofauti na VIP Engineering and Marketing Limited," alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru