Wednesday, 18 March 2015

Kinana awavaa wabunge CCM  • Awataka wasisubiri kuaibishwa, wajipime
  • Leizer aibua mapya, kubwaga manyanga

NA WAANDISHI WETU, LONGIDO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wabunge wake kujipima kama wanatosha kabla ya kuingia tena kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kazi ya kuwatumikia wananchi.
Sambamba na hiyo, CCM imewaonya wabunge kuanza kujiengua ili kulinda heshima zao ndani na nje ya Chama.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na wakazi wa Helendeke katika Mji Mdogo wa Namanga mkoani Arusha.
Alisema baadhi ya wabunge wamekuwa waking’ang’ania kuendelea kuwa wabunge bila kujipima kama wana uwezo au la.
Alisema hali hiyo imewafanya baadhi ya wabunge kukosa ubunge kwa kulinda aibu ikiwa ni pamoja na kushindwa katika uchaguzi.
Kwa mujibu wa Kinana, viongozi wengi wamekuwa na tabia ya kuendelea kutaka kutawala bila kujipima kama bado wananchi wanawahitaji au wamewachoka. 
Alisema hatua hiyo inatokana na viongozi hao kutofanya tathimini kuweza kubaini kama bado wanapendwa au wameshachokwa.
“Wapo baadhi hawajipimi kufahamu kama bado wananchi wanawapenda au la. Wanang’ang’ania madaraka mpaka waangushwe tena kwa aibu. Wanafahamu ni kuingia kuwa wabunge, lakini wakati wa kutoka hawajui.
“Wanaokupa madaraka ya kuendelea kuwa mbunge ni wananchi na hasa wana-CCM. Sasa kama hujipimi kuona kuwa wana-CCM wenzako wanaendelea kukupenda au la, utaondoka kwa aibu,” alisema Kinana.
Kinana alimmwagia sifa Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer, kwa kutangaza rasmi kuwa hatagombea tena ubunge katika jimbo hilo.
Alisema uamuzi wa Laizer unastahili kuigwa na wabunge wengine ambao wana tabia ya kuona majimbo kama mali yao binafsi.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Laizer alisema ameamua kutogombea kwa hiari yake ili kutoa fursa kwa nguvu mpya kuendeleza jahazi la maendeleo.
“Katibu Mkuu najua hujawahi kuona makabidhiano kati ya mbunge na mbunge na hili hutokana na wengi kuondolewa kwa kuangushwa katika uchaguzi. 
“Sasa nakuahidi kwa mara ya kwanza nitaanzisha utaratibu wa kukabidhi ofisi kwa mimi na mbunge ajae kwa kuwa ninaondoka mwenyewe,” alisema Laizer. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru