Thursday, 12 March 2015

Wazazi Mtwara watakiwa kuthamini elimu


Na Clarence Chilumba, Mtwara
SERIKALI imewataka wazazi na walezi mkoani Mtwara, kuwapeleka shule watoto wao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu. 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, wakati akizungumza na Uhuru mjini hapa.


Alisema elimu ndiyo itakayowasaidia vijana wa Mtwara kunufaika na  uchumi wa gesi, ambao unapatikana katika mkoa huo.
Alisema kama watoto wa mikoa ya kusini hawatapata elimu, wataishia kufanyakazi za chini, ambazo hazina hadhi.
Alisema kazi hizo hazitawawezesha vijana hao kunufaika, hivyo aliwaomba wazazi kutilia mkazo suala la elimu kwa watoto wao.
“Ndugu zangu bila kujibana na kujinyima, watoto wetu hawatasoma kwani sote sisi hapa tunaozungumza, tulikuwa watoto wa wazazi wa kawaida, lakini walijibana wakatusomesha na sasa hivi wanayaona matunda,” alisema Hawa.
Hawa, ambaye ni mbunge wa Mtwara Vijijini, aliipongeza wilaya yake kwa kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.
Hata hivyo, aliwataka watendaji na wazazi wasibweteke kwa matokeo hayo mazuri waliyoyapata, badala yake wakaze ‘buti’ ili waweze kushika nafasi za juu kitaifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru