Tuesday 17 March 2015

Kigoma, Rukwa wahofia wakimbizi kuandikishwa


WABUNGE wa mikoa ya Kigoma na Rukwa wameiomba serikali kuhakikisha wanadhibiti upigaji kura na uandikiswaji katika daftari la wapigakura watu wasio raia wa Tanzania walioko kwenye maeneo ya mipakani.
Kauli hiyo, ilitolewa, bungeni mjini hapa na wabunge, Josephine Genzabuke (Viti Maalum-CCM) na Ally Keisy, (Nkasi Kaskazini-CCM).
Akiuliza swali la nyongeza Gezabuke, alitaka kujua serikali imejiandaa vipi kuchukua hatua mahususi juu ya watu watakaotambuliwa kuwa  wakimbizi wakiwa wamejiandikisha kwenye  daftari la kudumu la wapigakura.
 Alisema zipo taarifa za kuwepo kwa wakimbizi 10 waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura mkoani kigoma.
“Serikali inachukua hatua gani kwa wakimbizi hao na wale ambao walipiga kura Karagwe, wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambao haukuwa na vitambulisho,” alihoji.
Kwa upande wake Keissy, alihoji ni hatua gani zitachukuliwa na serikali kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambao wamechaguliwa wakati si raia wa Tanzania katika jimbo lake.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, alisema serikali itakuwa tayari kushirikiana na kila mbunge ili kuchunguza masuala hayo na kuchukua hatua.
Mwanri alisema ni jukumu la viongozi wa vijiji, vitongoji, mitaa na wananchi kuwabaini watu ambao si raia au wakazi wa eneo husika na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.
“Kwa mujibu wa kanuni kabla ya siku ya uchaguzi, orodha ya wapigakura walioandikishwa hubandikwa katika kituo cha kupigia kura ili kuwawezesha wananchi wa eneo husika kubaini watu wasio na sifa wakiwemo wakimbizi,” alisema.
Alisema endapo wakimbizi waliothibitika kupiga au kupigiwa kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 katika mkoa wa Kigoma, serikali iko tayari kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru