Wednesday, 11 March 2015

Foleni ya wagonjwa ni tatizo


Na Happiness Mtweve, Dodoma
KITENGO cha Mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani hapa, kimeelemewa na wagonjwa huku ikiwa na mashine moja.
Daktari Bingwa wa Mionzi, Philimon Saigodi, aliwaeleza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, kuwa hiyo imekuwa kero kubwa kwa wagonjwa.
Alisema wanahudumia wagonjwa 60 mpaka 70 kutoka katika mikoa ya Singida, Dodoma na wilaya za Kiteto na Manyoni.
Alisema kitengo hicho ni kikubwa na kina wagonjwa wengi, ambao wanaongezeka siku hadi siku, hivyo kujikuta kikiemewa na kushindwa kuhudumia wagonjwa kikamilifu.
“Mashine ya mionzi tunayo moja tu, imekuwa ikizidiwa na kupata moto, ambapo tunalazimika tuizime ipumzike ndipo tuiwashe tena huku wagonjwa wakiwa wamesubiri kwenye foleni,” alisema.
Aidha, chumba hicho cha kupimia mionzi hakina kiyoyozi, ambacho kingesaidia mashine hiyo kupoa.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe, alisema, serikali ina mpango wa kupeleka mashine mpya za mionzi katika hospitali kadhaa nchini.
“Mashine tunazotaka kuzileta zitakuwa za kisasa kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo, ambalo limedumu kwa muda sasa,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru