NA MWANDISHI MAALUM, BLANTYRE
WAKATI Rais Jakaya
Kikwete akitangaza vita na mtandao hatari unaojihusisha na utekaji na mauaji ya
walemavu wa ngozi (albino), matukio hayo kwa sasa yameshika kasi nchini Malawi.
Juzi, wakati akihutubia taifa
katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema serikali
itahakikisha inasambaratisha mtandao huo na kuwataka watanzania wote kushiriki
kwenye vita hiyo.
Hata hivyo, imebainika
kuwa baada ya serikali kuunda kikosi maalumu cha kukabiliana na mtandao huo,
matukio ya kuuawa kwa albino yamehamia nchini Malawi.
Habari za kuaminika
zinasema tayari walemavu wa ngozi watatu wameuawa katika kipindi cha miezi
mwili, hatua ambayo inatajwa kuwa ni mbaya na serikali imeanza kukabiliana na
wimbi hilo.
Rais wa Chama cha
Maalbino nchini Malawi (APAM), Boniface Massah, alisema hofu imetanda katika
kila kona na watu wenye ulemavu wamekuwa wakiishi kwa hofu kuhofia maisha yao.
Alisema chama chake
kinahofu kwamba kuongezeka kwa mauaji hayo, kunatokana na udhibiti na hatua
kali zilizotangazwa na Tanzania dhidi ya mauaji ya albino.
"Hivi sasa hatuna amani, tunaishi kwa shaka kwa kuwa wakati wowote tunaweza kunaswa na kuuawa," alisema.
Akizungumzia moja ya
matukio ya vifo vitatu vilivyotokea mwaka huu, Massah alisema mama mmoja ambaye
hakumtaja jina, alikutwa ameuawa na kukatwa baadhi ya viungo vyake.
Baadhi ya viungo
vilivyokatwa kutoka kwa mwanamke huyo ni kichwa, mikono na miguu ambavyo
vinaaminika kutumika kwa imani za kishrikina.
Kasi hiyo inaonekana kuwa
kali ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita ambapo, maalbino wawili
waliripotiwa kuuawa.
Katika kipindi cha hivi
karibuni, kumekuwepo na matukio ya kutekwa na kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa
ngozi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kusababisha hofu kubwa.
Kwa mujibu wa Shirika la
Kutetea Haki za Maalbino la Under The Same Sun (UTSS), watu 140 wenye ulemavu
huo wameshauawa kati ya mwaka 1998 na 2015 kwenye nchi 25 za Afrika.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru