Thursday, 26 March 2015

Wanaojipitisha kusaka uongozi watakiwa kusubiri


NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM,  Dk. Edmund Mndolwa, amesema viongozi wanaojipitisha kwa ajili ya kutaka uongozi ndani ya chama, wanawachanganya wananchi, hivyo wasubiri muda ufike.
Aidha, amewataka baadhi ya viongozi wa CCM, wanaowatumia viongozi wa dini kuwatetea wakati wanapokosolewa, kuacha mara moja tabia hiyo.
Dk. Mndolwa alisema hayo mjini Dar es Salaam, jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema muda wa kupata wagombea ndani ya chama haujafika, hivyo si vyema kwa baadhi ya makada kuanza kujipitisha kwa ajili ya kusaka uongozi na wanaofanya hivyo wanawachanganya wananchi.
Dk. Mndolwa alisema katika siku za hivi karibuni, baadhi ya viongozi wanawatumia viongozi wa dini kuwatetea wanapokosolewa na kwamba tabia hiyo haikubaliki.
Hata hivyo, alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, pamoja na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwa kukiimarisha chama.
Alisema ziara zinazofanywa na viongozi hao zimekirudisha chama kwenye hadhi yake na kwamba viongozi wengine wanapaswa waige mfano wa viongozi hao.
“Katibu Mkuu wetu (Kinana), pamoja na Nape wanafanya kazi kubwa ya kukijenga chama, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuiga mfano huo. Ziara zao zimekiimarisha chama na kuleta matumaini mapya,” alisema.
Wakati huo huo Mndola alimpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa  CCCM,  Rais Jakaya Kikwete, kwa uamuzi wake wa busara wa kufuta ada za shule.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru