NA VICTOR MKUMBO
BAO pekee lililofungwa dakika ya 51 na
Emmanuel Okwi, limeiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, katika
mchezo wa Ligi Kuu ulioikutanisha timu hiyo na Yanga.
Okwi alipachika bao hilo kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia
Bartez aliyetoka nje ya lango na mpira huo kujaa moja kwa moja wavuni.
Ushindi huo unaipa jeuri Simba ya kuendelea kuwatambia mahasimu wao ambao
wamekuwa wakiibeza Simba baada ya kufanya
vibaya katika baadhi ya michezo yake ya ligi.
Katika mchezo huo, uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilianza pambano hilo kwa kasi na kuonyesha
dalili ya kupata ushindi.
Dakika ya pili Simba ilifanya shambulizi kali kupitia kwa Ibrahim Ajib
kabla ya mabeki wa Yanga kuokoa hatari hiyo.
Yanga ilijibu shambulizi hilo dakika ya saba kupitia kwa Simon Msuva,
aliyeachia shuti hafifu lililojaa
mikononi mwa kipa Ivo Mapunda.
Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku Simba ikicheza mipira
ya kuotea na kutafuta mabao ya mapema.
Dakika ya 18 nusura Msuva aipatie Yanga bao baada ya kuwachambua mabeki
wa Simba na kuachia shuti lililookolewa na beki wa Simba.
Simba ndiyo iliyoonyesha uhai mkubwa kwa kucheza kwa kuelewana na
kufanikiwa kutawala mpira kwa asilimia kubwa.
Yanga nayo ilijizatiti na kutafuta nafasi ambapo dakika ya 19, 24, 36 na
41 ilipata nafasi za kufunga kupitia kwa
Amis Tambwe, Danny Mrwanda na Mrisho Ngasa, lakini Mapunda na mabeki wake
waliondosha hatari zote langoni mwao.
Simba iliendelea kufanya mashambulizi na kutafuta mabao mengine ya
kufunga, ambapo dakika ya 80, Okwi alipata nafasi nyingine ya kufunga, lakini
shuti alilopiga lilitoka pembeni ya goli.
Hadi mchezo huo unamalizika, Simba ilitoka kifua mbele na kuendeleza
rekodi ya kuwafunga wapinzani wao kila wanapokutana.
Katika mchezo huo, mwamuzi Martin Saanya aliwaonyesha kadi za njano Abdi
Banda, Juuko Murshid, Haruna Niyonzima, Nadir Haroub na Amis Tambwe baada ya
kuwachezea vibaya wenzao.
Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na Yanga katika mchezo wa raundi ya kwanza
kabla ya kushinda mabao 2-0, katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
Simba: Ivo Mapunda, Kessy Ramadhan, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka,
Juuko Murshid, Abdi Banda, Ramadhan Singano, Jonas Mkude, Ibrahim Ajib/Elias
Maguri, Said Ndemla na Emannuel Okwi.
Yanga: Ally Mustafa, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin
Yondan, Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe, Mrisho
Ngasa/Sherman na Danny Mrwanda.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru