Friday, 27 March 2015

Wanafunzi wamkana Lowassa


NA  WAANDISHI WETU
VIONGOZI wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu mjini  Dodoma, wamekanusha kumchangia fedha na kumwomba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kugombea urais. 
Pia wamewataka wanafunzi wenzao kujitambua na kutumia muda wao kwa mambo ya msingi kwa ustawi wao na taifa, badala ya kujingiiza katika mambo ya siasa za aina hiyo.
Taarifa iliyotumwa na Uongozi wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma, ilisema kundi lilijikusanya Machi 22, mwaka huu, nyumbani kwa Lowasa, likijitambulisha kuwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma na kutoa matamko mbalimbali pamoja na  kuutangazia umma kuwa wanamtaka agombee urais .
Taarifa hiyo ilisema jambo hilo si la kweli na wanalaani vikali kitendo cha watu wachache kwenda kwa Lowassa na  kujifanya wanafunzi wa vyuo vikuu vya mkoani Dodoma.
“Sisi kama wasomi ambao jamii inatutegemea hatuwezi kuandamana na kujikusanya katika nyumba ya kiongozi yeyote kumwomba agombee urais wakati tunajua fika hatuhusiki na uteuzi wa wagombea ndani ya taasisi yao,” ilisema taarifa hiyo.
Kilichofanyika ni kuudanganya umma na taasisi zake kupitia kivuli cha  vijana wachache kutoka vyuo vya dodoma waliolipwa fedha ili waweze kufanya jambo hilo.
Ilisema taarifa hiyo kuwa Mkoa wa Dodoma una vyuo takribani vinane  na jumla ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo ni zaidi ya 35,000 ambapo Chuo Kikuu cha Dodoma peke yake, kina wanafunzi wasiopungua 22,000, kulinganisha na watu 230 waliojikusanya nyumbani kwa mbunge huyo, wakiwemo wamachinga na wenyeviti wa jumuia ya wazazi. 
Taarifa hiyo iliongeza kwua licha ya wenyeviti hao waliotoka katika mikoa mbalimbali na wamachinga, idadi ya wanafunzi waliokuwepo katika tukio hilo hawazidi 150 ambayo ni sawa na asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma.
“Kwa akili ya kawaida, asilimia iliyokuwepo pale ni ndogo hivyo wanashangazwa na dhambi wasiyoifanya ambapo wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma hivi sasa wako katika muhula mpya wa masomo.
“Sisi kama vijana wasomi na tunaotegemewa na jamii zetu tutakusanyika na kujadili na kuchambua changamoto mbalimbali zinazotukabili na kwa mwanasiasa ambaye uadilifu wake unatiliwa shaka,” ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza hawakubaliani na wanafunzi wachache kuchafua na kuwapaka matope maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu hivyo ambao hawajahusika na tukio hilo, si haki na haikubaliki.
Pia ilisema wanatoa wito kwa wanafunzi wote nchini na jamii yote kwa ujumla kuacha kuzungumzia maamuzi ya mtu binafsi na wasikubali kutumika kwa wanasiasa wanaotumia fedha kwa ajili ya kuwalaghai.

NAPE AMPONGEZA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwa kusitisha utaratibu wa kuyapokea makundi yanayokwenda kumshawishi agombee urais, anaripoti THEODOS MGOMBA kutoka Dodoma.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Same.
Kauli hiyo ya Nape inakuja siku moja tu baada ya Lowassa kutangaza kusitisha makundi mbalimbali kwenda na kumshauri kugombea nafasi hiyo.
Nape alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya CCM ambayo yeye ni mmoja wa wanachama wake.
Alisema alichokuwa akikifanya Lowassa ni kuanza kampeni mapema  kabla ya wakati jambo ambalo ni ni uvunjifu wa kanuni, katiba na taratibu za Chama.
Kwa upande wa wapambe, Nape alisema makada wa wanachama wanaotaka  kugombea urais kupitia CCM, ni lazima wafuate taratibu za kichama.
Alisema ni vyema wataka urais hao wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao kwa kuwa wanaweza kuwasababishia kukosa sifa.
Aaliwashauri wanaotaka kugombea nafasi hiyo ya urais  kupitia CCM kutowasiliza wapambe wao kwa kila wanachoambiwa maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha sifa za kugombea urais.
Nape alisisitiza kusisitiza kuwa ni muhimu kwa makada wote kuhakikisha wanaheshimu kanuni, taratibu na miiko ya Chama hicho ili wawe salama kinyume na hapo watajipoteza sifa.
Aidha Nape alisema CCM itatenda haki kwa wanachma wote watakaofuata taratibu katika uchaguzi huo bila kujali ni nani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru