Tuesday 17 March 2015

Mbunge aijia juu Wizara ya Ardhi


Na Happiness Mtweve, Dodoma
MBUNGE wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, ameiomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kutoa muda wa kutosha kuwahudumia wananchi.
Akiuliza swali bungeni jana mjini hapa, Mangungu alisema kumekuwepo na malalamiko ya wananchi kutopata muda wa kutosha kupata huduma mbalimbali kutoka wizarani hapo.
Mangungu alisema wizara hiyo ni nyeti na inategemewa na Watanzania wote kushughulikia huduma mbalimbali katrika eneo la ardhi, nyumba na makazi.
Alihoji kwa nini serikali haiongezi muda wa kazi kwa watumishi wa wizara hiyo ili kuhudumia wateja wengi ikiwa ni pamoja na kutatua  changamoto mbalimbali.
“Kuna tatizo la kuwapiga kalenda wananchi wanapofika kwenye wizara na idara za ardhi, kwa ajili ya kupata huduma,” alisema.
Akijibu swali la msingi na maswali ya nyongeza ya Mangungu, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angellah Kairuki, alisema wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, wizara imekuwa ikiwakemea watumishi wake kwa kutoa huduma kwa ubabaishaji.
Alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuzorota au kutotimiza wajibu wake.

Angella alisema wizara hutoa huduma kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kwa siku zote za kazi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru