Monday, 16 March 2015

Sefue: Ubunifu kichocheo cha maendeleo




NA WILLIAM SHECHAMBO
WATANZANIA wametakiwa kujijengea utamaduni wa kubuni mambo mbalimbali ya kimaendeleo kwa kutumia sayansi na teknolojia kwa kuwa hakuna maendeleo bila ubunifu.
Balozi Ombeni Sefue
Viongozi wa nchi wamekuwa wakionyesha njia katika ubunifu kwenye sekta zote tangu awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, mpaka sasa ambapo maendeleo yanazidi kuonekana wakati nchi ikielekea kwenye uchumi wa kati.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitoa rai hiyo Dar es Salaam jana, alipokuwa akifungua warsha iliyopewa jina la 'maabara' ya wiki tatu ya wadau wa sayansi, teknolojia na ubunifu inayofanyika kwenye hoteli ya Kunduchi Beach.
Alisema historia inaonyesha nchi zenye watu wanaojituma katika ubunifu wa kiteknolojia kwa miaka 50 iliyopita, hasa za Asia na Amerika Kusini, zimeendelea haraka kiuchumi.
Balozi Sefue alisema serikali tangu ianzishe mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), imejiingiza kwenye utaratibu wa kutumia maabara kuwakutanisha wataalamu wa sekta fulani, ili wajadiliane na kutoka na suluhisho la changamoto zinazowakabili katika sekta yao.
Alisema kwenye sekta ya mawasiliano, sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ujumla, serikali kupitia wizara husika imeandaa warsha hiyo kuangalia jinsi gani tamko la Rais Jakaya Kikwete, alilolitoa 2009 kwa wizara na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), limetekelezwa.
Tamko hilo lilitaka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na shirika hilo kupitia upya mfumo wa mawasiliano, sayansi na teknolojia ili kuwa bora na wenye kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, alisema ni ukweli usiofichika kuwa ubunifu wa teknolojia kwa miaka mitano iliyopita, umetoa mchango mkubwa kwa baadhi ya nchi duniani kutoka kwenye uchumi wa chini kuwa na uchumi wa kati ambao unasababishwa na uwepo wa viwanda vizuri na watu wenye uchumi mzuri.
Katibu Mkuu Kiongozi alisema serikali ya awamu ya nne imeonyesha jitihada kubwa kwenye kuwawezesha wananchi kujitegemea kiuchumi kwa kuboresha na kujenga miundombinu mbalimbali iliyobuniwa kisayansi.
Baadhi ya jitihada hizo ni kuanzishwa kwa kitamizi cha teknolojia kinachosimamiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambacho kinatoa fursa kwa vijana kujifunza ubunifu ili kuisaidia nchi kwenye nyanja mbalimbali.
Balozi Sefue alisema vitamizi hivyo kwa nchi kubwa kama Tanzania vinatakiwa kuwa vingi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa teknolojia kwa muda mfupi watakaotawanywa kwenye kila sekta nchini.
Alisema malengo ya sasa kwa msaada wa BRN ni kuitumia teknolojia kufika uchumi wa kati kabla ya 2025 hivyo kila mwananchi kwa nafasi yake, taasisi na serikali ina kazi kubwa kulifanikisha lengo hilo.
Aliwataka wataalamu na wadau wanaohudhuria warsha hiyo inayosimamiwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia baada ya wiki tatu kutoka na mapendekezo ya namna serikali kwa kushirikiana na wadau itatoa umadhubuti kwenye mfumo na kiutendaji na kisera kwa kupitia teknolojia ya mawasiliano.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru