Tuesday 10 March 2015

Polisi yawanasa 15 kiganja cha albino



NA WILLY SUMIA, SUMBAWANGA
POLISI mkoani Rukwa wanawashikilia watu 15, wakiwemo waganga wa kienyeji saba kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio la kukatwa kiganja cha mtoto Baraka Cosmas.
Baraka (6), ambaye ni mlemavu wa ngozi, alikatawa kiganja cha mkono mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akiwa amelala na mama yake usiku.
Watuhumiwa hao walitiwa mbaroni kufuatia msako mkali unaoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, ikiwa ni muda mfupi baada ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema kikosi maalumu cha polisi kinaendelea na msako mkali kuhakikisha mtandao wote wa utekaji na mauaji ya albino unatiwa mbaroni.
Alisema baada ya kutiwa mbaroni watuhumiwa hao, walianza kutajana hadi kufikia 15, ambao wote kwa sasa wanaendelea kuhojiwa kabla ya kupandishwa kizimbani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Kamanda Mwaruwanda aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Mwendesha William (30), Masunga Bakari (50), David Kiyenze (45) na Ngolo Masinga (47), wote wakazi wa Kijiji cha Kaoze wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Wengine ni Mageta Shimba (46), Pascal Jason (40), Mnyika Managa pamoja na baba mzazi wa Baraka, Cosmas Yolam (32).
Waganga wanaoshikiliwa ni Eliza Malongo (36), Sodeli Malimbo, maarufu kama Chuchi (66), Akobo Chinzwe (50), Leonard Samson (59) na Inglibert Kasinde (45).
Wengine ni Boniphace Chalya (49), Charles Misalaba (47) na Julius Simbamwene (40).
Alisema waganga wa jadi hao walikutwa na vifaa vya kuagua na kupigia ramli pamoja na nyara za serikali kama vile mayai ya mbuni, kucha za chui, ngozi ya pakapori, kobe aliyekaushwa, ngozi ya chui na nywele zinazosadikiwa ni za binadamu.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru